Haaland amkataa Kane

Muktasari:

  • Haaland aliibuka shujaa kwenye mchezo wa Ligi Kuu England juzi Jumamosi usiku na alitupia mabao manne kwenye ushindi wa mabao 5-1 , huku lingine likifungwa na Julian Alvarez na la kufutia machozi la Wolves likifungwa na Hwang Hee-chan.

MANCHESTER, ENGLAND: Mshambuliaji wa Manchester City, Erling Haaland amesema wala hajali kuhusu maneno ya mchezaji wa zamani wa Manchester United Roy Keane aliyemsifia na kumkandia kuhusu kiwango chake.

Haaland aliibuka shujaa kwenye mchezo wa Ligi Kuu England juzi Jumamosi usiku na alitupia mabao manne kwenye ushindi wa mabao 5-1 , huku lingine likifungwa na Julian Alvarez na la kufutia machozi la Wolves likifungwa na Hwang Hee-chan.

Kean baada ya Haaland kuonyesha kiwango kibovu dhidi ya Arsenal, Machi mwaka huu, alisema :”Uwezo wake wa kucheza kijumla ni mdogo sana na sio tu leo (kwenye mechi hiyo), nafikiri ndivyo alivyo, anakuwa hatari anapokuwa mbele ya goli tu, lakini timu ikiwa ina mpira na inatengeneza mashambulizi kiwango chake ni kidogo, nafikiri anatakiwa abadilike kwa sababu anaonekana kama mchezaji wa Ligi Daraja la tat,” alisema na kuongeza, “Lakini kuja kubadilika na kuwa bora kwa namna ninavyosema, itachukua muda sana inawezekana ikawa hata miaka kadhaa ijayo.”

Hata hivyo, staa wa Norway ambaye amefikisha mabao 25, amemjibu akisema anachokiwaza kwa sasa ni kushinda  akiwa anaongoza katika vita ya kuwania ya ufungaji bora Ligi Kuu England msimu huu.

“Sijali sana kuhusu huyo mtu, kwa hiyo hainishughulishi sana, tunachotakiwa sasa ni kushinda tu mechi, kama hivi sasa tumeshinda, tunaenda kupumzika na kusubiri mechi ijayo dhidi ya  Fulham,” alisema Haaland.

Baada ya kauli hiyo Haaland akarudi na kuuwasha moto dhidi ya Nottingham Forest mwishoni mwa mwezi uliopita na Keane akasema anaona ameimarika sana na sasa amekuwa kama mchezaji wa Ligi Daraja la kwanza kutoka Daraja la tatu.