Guehi, FC Bayern Munich kuna jambo
Muktasari:
- Beki huyo wa kimataifa wa England, Guehi alikaribia kabisa kuondoka Selhurst Park kwenye dirisha lililopita kabla ya dili lake la kwenda Liverpool kukwama kwenye siku ya mwisho ya kufungwa kwa dirisha hilo la uhamisho.
LONDON, ENGLAND: MAWAKALA wa beki wa kati, Marc Guehi wameripotiwa kukutana na mabosi wa Bayern Munich kwa ajili ya kufanikisha uhamisho wa bure kwenye dirisha lijalo la majira ya kiangazi baada ya kufanya uamuzi wa kuachana na Crystal Palace.
Beki huyo wa kimataifa wa England, Guehi alikaribia kabisa kuondoka Selhurst Park kwenye dirisha lililopita kabla ya dili lake la kwenda Liverpool kukwama kwenye siku ya mwisho ya kufungwa kwa dirisha hilo la uhamisho.
Guehi bado amesisitiza mpango wake wa kuondoka na kocha wa Palace, Oliver Glasner alifichua beki huyo hana mpango wa kusaini mkataba mpya.
Mkataba wa beki huyo utafika tamati mwishoni mwa msimu wa 2025-26 na kuna timu kibao zinafukuzia huduma yake. Moja ya timu hizo ni miamba ya soka ya Ujerumani, Bayern Munich na ripoti zinafichua tayari mazungumzo yameanza vizuri.
Bayern inatafuta beki wa kati mpya endapo kama Dayot Upamecano au Kim Min-Jae mmoja wao ataondoka kwenye klabu hiyo mwishoni mwa msimu.
Ripoti zinafichua ofisa mmoja wa Bayern Munich, Max Eberl, alikutana na wakala wa Guehi, Gordon Stipic huko Munich kwa ajili ya kujadili uwezekano wa kutokea kwa dili hilo.
Wakati Bayern ikiwa kwenye mbio za kumsajili beki huyo, wasiwasi ni kwamba huenda wakakabiliana na mchuano mkali kutoka kwa Liverpool, ambao bado wanamhitaji Guehi baada ya kumkosa kwenye dirisha lililopita. Real Madrid nayo inafukuzia huduma ya Guehi kimyakimya.
Guehi ameanzishwa kwenye mechi zote nane za Ligi Kuu England ilizocheza Palace msimu huu, akifunga mara moja na kuasisti mara moja pia.