Ndo hivyo, Guehi anaondoka
Muktasari:
- Bosi huyo Muaustria alifichua kwamba Guehi, ambaye ni beki wa kimataifa wa England hatasaini mkataba mpya na kwamba ataondoka bure mwishoni mwa msimu.
LONDON, ENGLAND: KOCHA wa Crystal Palace, Oliver Glasner amethibitisha beki wa kati Marc Guehi ataondoka kwenye klabu hiyo ikiwa ni miezi michache imepita tangu alipokwama kujiunga na Liverpool kwenye dirisha lililopita la uhamisho wa majira ya kiangazi.
Bosi huyo Muaustria alifichua kwamba Guehi, ambaye ni beki wa kimataifa wa England hatasaini mkataba mpya na kwamba ataondoka bure mwishoni mwa msimu.
Liverpool ilishuhudia dili lake la kumsajili Guehi siku ya mwisho ya kufungwa kwa dirisha la usajili likifungwa kwa kuwa Palace haikuwa imepata mbadala wake.
Beki wa Brighton, Igor Julio alikuwa kwenye hatua za mwisho kabisa kukamilisha uhamisho wa kutua Selhurst Park, lakini alikubali kwenda kwa mkopo West Ham.
Kwa sasa, Guehi ataendelea kubaki Selhurst Park walau hadi Januari, ambapo Palace inaweza kumuuza ili kupata chochote kitu kuliko kumruhusu aondoke bure.
Kinachoelezwa ni kwamba Palace inaweza kufikiria kumuuza beki huyo kwenye dirisha la majira ya baridi ili kupata pesa.
"Nadhani Marc alishatuamini kwamba hawezi kusaini mkataba mpya, hivyo hatakuwapo msimu ujao," amesema Glasner.
"Klabu inamtaka abaki. Imempa ofa ya mkataba mpya. Lakini, amesema; 'Hapana, nataka changamoto mpya'.Na hilo ni kawaida."
Kuhusu Liverpool kama itafanya mchakato wa kwenda kunasa saini ya Guehi wakati wa dirisha la Januari ndicho kitu kinachosubiriwa. Huko nyuma iliwahi kuripotiwa kwamba haina mpango wa kurudi kwenye mchakato wa kumsajili beki huyo itakapofika Januari.