Guehi afikiria kutema unahodha
Muktasari:
- Guehi alijiandaa kujiunga na Liverpool kwenye siku ya mwisho ya kufungwa kwa dirisha la usajili, wakati mwenyekiti wa Palace, Steve Parish alipopingana na kocha Oliver Glasner kukubali ofa ya Pauni 35 milioni ya kumuuza beki huyo huko Anfield.
LONDON, ENGLAND: BEKI wa kati, Marc Guehi ameripotiwa kufikiria mpango wa kuvua kitambaa cha unahodha kwenye kikosi cha Crystal Palace akiwa na hasira ya klabu kuzuia uhamisho wake Liverpool.
Guehi alijiandaa kujiunga na Liverpool kwenye siku ya mwisho ya kufungwa kwa dirisha la usajili, wakati mwenyekiti wa Palace, Steve Parish alipopingana na kocha Oliver Glasner kukubali ofa ya Pauni 35 milioni ya kumuuza beki huyo huko Anfield.
Guehi alifanyiwa vipimo vya afya London na ilikuwa asafiri kwenda Merseyside kujiunga na Liverpool. Lakini, Parish alibadili mawazo dakika za mwisho baada ya kocha Glasner kutishia kujiuzulu kwa sababu hakukuwa na mbadala wa Guehi.
Palace ilikubaliana kumchukua kwa mkopo Igor Julio kutoka Brighton, lakini beki huyo Mbrazili alichagua kwenda kujiunga na West Ham United.
Jambo hilo lilikuwa na madhara kwenye uhamisho wa Guehi, ambaye sasa ilibidi abaki ili kumfanya kocha Glasner naye abaki kwenye kikosi.
Ripoti zinafichua kwamba Guehi hakufurahishwa kabisa na kilichotokea, wakati mkataba wake kwenye klabu hiyo yenye maskani yake Selhurst Park ukifikia tamati Juni 2026.
Kinachoripotiwa ni kwamba Guehi hatakubali ofa yoyote ya mkataba mpya kwenye kikosi hicho cha Palace, hivyo itakapofika Januari atakuwa huru kusaini mkataba wa awali kwenye klabu za nje ya England.