Guardiola: Huyu Cherki anajua sana
Muktasari:
- Guardiola amesema hilo akimzungumzia staa huyo Mfaransa wakati kikosi chake kilipokuwa kikijiandaa na mchezo wa Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Villarreal.
MANCHESTER, ENGLAND: KOCHA wa Manchester City, Pep Guardiola akiri amekuwa akikoshwa sana na mchango unaofanywa na staa wake mpya, Rayan Cherki katika kikosi hicho cha Etihad.
Guardiola amesema hilo akimzungumzia staa huyo Mfaransa wakati kikosi chake kilipokuwa kikijiandaa na mchezo wa Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Villarreal.
“Rayan ni mmoja wa wachezaji wenye vipaji vikubwa niliowahi kuwaona kwenye maisha yangu ya ukocha,” amesema Guardiola.
“Kipaji chake ni kiboko. Ishu ni jinsi gani ametulizana na namna anavyopaswa kusoma mchezo unavyokwenda. Alicheza vizuri kwenye Kombe la Dunia la Klabu, lakini alikuwa na mapumziko ya wiki chache. Amekuwa na furaha kubwa mpira unapokuja kwenye miguu yake.
“Anacheza bila ya presha, amekuwa akicheza kama mchezaji wa mitaani. Amekuwa akiutaka mpira muda wote.
“Lakini, alihitaji muda mfupi wa kujiweka sawa, alihitaji muda kidogo kwa sababu soka unapaswa kujifunza namna ya kucheza na wachezaji wenzako. Lakini, huyu ni aina ya wachezaji wenye akili kubwa. Wanang'amua kila jambo mapema sana.”