Guardiola awapa msala mabosi EPL

Muktasari:
- Man City ilicheza na Crystal Palace kwenye fainali ya Kombe la FA, Jumamosi, kisha itakabiliana na Bournemouth ndani ya saa 72 katika mechi ya lazima ushindi ili kuwamo kwenye Top Five inayotoa tiketi ya kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao kwa kupitia kwenye Ligi Kuu England.
MANCHESTER, ENGLAND: PEP Guardiola amepeleka lawama zake kwenye Ligi Kuu England akilalamika wanaiweka Manchester City kwenye hali ngumu ya kufikia ndoto za kufuzu Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao.
Man City ilicheza na Crystal Palace kwenye fainali ya Kombe la FA, Jumamosi, kisha itakabiliana na Bournemouth ndani ya saa 72 katika mechi ya lazima ushindi ili kuwamo kwenye Top Five inayotoa tiketi ya kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao kwa kupitia kwenye Ligi Kuu England.
Guardiola, ambaye timu anayoinoa Man City ipo kwenye nafasi ya sita kwenye msimamo wa Ligi Kuu England, iliomba mechi hiyo ya Bournemouth isogezwe mbele kwa saa 24, lakini aligomewa.
Wakati huo, Ligi Kuu England ilibadilisha mechi za Tottenham na Manchester United kuchezwa Ijumaa dhidi ya Aston Villa na Chelsea Ijumaa ili kutoa nafasi kwa timu hizo kujiandaa na fainali ya Europa League itakayofanyika Jumatano ijayo huko Bilbao, Hispania.
Guardiola alisema: "Tottenham imecheza na Aston Villa Ijumaa, kwa sababu ya fainali ya Europa League. Uamuzi mzuri, sisemi kwa dhihaka, lakini Ligi Kuu England imefanya uamuzi mzuri.
"Tulicheza mara zote robo fainali na nusu fainali ugenini siku za Jumatano na tulikuwa na mechi Jumamosi. Msimu huu, tulicheza Jumapili na hatukuhitaji siku ya ziada. Ningependelea kucheza Jumatano. Tumekuwa tukipambana na hili kila msimu kwa miaka tisa sasa. Tutacheza Jumanne usiku dhidi ya timu ngumu. Bournemouth inapambania nafasi Europa League, lazima tukabiliane."
Kwenye fainali ya Kombe la FA, Guardiola aliweka milango wazi kwa kiungo wake Rodri kurejea kwenye kikosi baada ya kuwa nje ya uwanja kwa muda mrefu tangu alipofanyiwa upasuaji wa goti.