Guardiola amchomoa De Bruyne kimtindo
Muktasari:
- De Bruyne amekuwa kwenye kikosi cha Man City tangu mwaka 2015 na amekuwa sehemu ya mafanikio makubwa ya timu hiyo chini ya kocha Guardiola, lakini mkataba wake utafika mwisho Juni mwaka huu.
MANCHESTER, ENGLAND: SUPASTAA, Kevin De Bruyne atalazimika kutazama upya mpango wake wa kutaka kustaafu soka kwenye kikosi cha Manchester City baada ya kauli ya kocha Pep Guardiola kuhusu mahitaji ya soka la kisasa.
De Bruyne amekuwa kwenye kikosi cha Man City tangu mwaka 2015 na amekuwa sehemu ya mafanikio makubwa ya timu hiyo chini ya kocha Guardiola, lakini mkataba wake utafika mwisho Juni mwaka huu.
Lakin, umuhimu wake kwenye timu imekuwa mdogo kwa kipindi cha miezi 18 iliyopita kutokana na kusumbuliwa sana na majeruhi. Kiungo huyo mwenye umri wa miaka 33 alikoseka uwanjani kwa karibu miezi miwili kuanzia Sptemba kutokana na kusumbuliwa na maumivu ya nyonga na msimu uliopita alicheza mechi 26 tu kutokana na kusumbuliwa na maumivu ya misuli.
Na sasa ni mmoja wa wachezaji ambao Guardiola huenda akawafungulia mlango mwishoni mwa msimu huu. Kwa hali ilivyo, De Bruyne anaweza asisainishwe mkataba mpya kwenye timu hiyo, hivyo anachopaswa ni kuchangamkia tu fursa ya kwenda kujiunga na klabu za Saudi Pro League kwenye dirisha lijalo.
“Lazima tuangalie uhalisia,” alisema Guardiola kabla ya mechi ya Liverpool, Jumapili.
"Lazima tukae kitako na madaktari, fizio, wachezaji na mawakala na tuwekane wazi kama mchezaji hachezi kila mwezi, au anacheza mara tatu ndani ya miezi miwili. Huo ndio ukweli. Tuna wachezaji wengi na wengine hawana mambo kama hayo na wanaweza kucheza, unasafiri nao na hakuna tatizo lolote.
“Siku zote tunataka kuwa timu shindani kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya. Tunahitaji kufika robo fainali, nusu fainali na fainali. Kama tunafikiria mambo mazuri kwa miaka ya baadaye, tunahitaji wachezaji ambao watakuwa fiti kwa ajili ya kuchezea timu.”