Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Greenwood asababisha bosi kuondoka Marseille

GREENWOOD Pict

Muktasari:

  • Kiongozi huyo wa klabu hiyo ya Ligue 1 ameondoka wakati mvutano ukiongezeka Marseille katika kipindi cha vurugu ambacho pia kimeshuhudiwa kuondoka kwa kocha Roberto De Zerbi.

MARSEILLE, UFARANSA: MKURUGENZI wa michezo wa Olympique Marseille, Medhi Benatia, amejiuzulu wadhifa wake kufuatia taarifa za hivi karibuni kuhusu mgogoro wake na mchezaji Mason Greenwood.

Kiongozi huyo wa klabu hiyo ya Ligue 1 ameondoka wakati mvutano ukiongezeka Marseille katika kipindi cha vurugu ambacho pia kimeshuhudiwa kuondoka kwa kocha Roberto De Zerbi.

De Zerbi aliondoka kufuatia kipigo cha mabao 5-0 kutoka kwa wapinzani wao Paris Saint-Germain, wakati timu ikiwa katika nafasi ya nne kwenye msimamo wa ligi na pia baada ya kutolewa kwa njia ya kusikitisha katika hatua inayofuata ya Ligi ya Mabingwa Ulaya.

Benatia, mchezaji wa zamani wa kimataifa wa Morocco, aliyewahi kuwa na mafanikio makubwa katika klabu kama Bayern Munich, AS Roma na Juventus, amesema ameondoka kutokana na matatizo yanayoendelea.

Katika taarifa yake amesema: "Tangu nifike kwenye hii klabu, nimefanya kazi kwa moyo wote nikiwa na lengo moja tu: kuirejesha Olympique de Marseille mahali pake stahiki. Naijua klabu hii, najua inachohitaji na shauku inayoiendesha.

"Leo bado tupo kwenye ushindani. Lengo la kufuzu Ligi ya Mabingwa Ulaya bado linawezekana na bado tunapigania kuleta nyumbani Coupe de France. Licha ya vikwazo vya hivi karibuni na matukio ya kusikitisha, mradi unaendelea vizuri uwanjani, lakini siwezi kupuuza hali ya sasa.

"Ninahisi kutoridhika kunazidi kuongezeka na mawasiliano yameharibika, jambo ninalolijutia sana. Hapa Marseille, matokeo ndiyo kipimo pekee cha kweli. Mnanijua kwa uwazi na ukweli wangu. Kutokana na mvutano unaozunguka uongozi, nimewasilisha barua yangu ya kujiuzulu, kwa sababu naamini klabu iko juu ya mtu binafsi, na sitaki uwepo wangu uwe kikwazo kwa maendeleo ya taasisi hii."

Imeelezwa katika wiki za hivi karibuni kuwa Benatia alikuwa amehitilafiana na Greenwood. Mwingereza huyo yupo katika klabu hiyo ya Ufaransa tangu 2024 na amejiimarisha kama mchezaji muhimu, huku akipata uungwaji mkono hadharani kutoka kwa De Zerbi. Hata hivyo, inaripotiwa kuwa wawili hao walikuwa hawaelewani.

Kwa mujibu wa gazeti la L'Equipe, wawili hao walikuwa wakipuuzana hadharani, huku Benatia (38) akidaiwa kuwa mkosoaji mkubwa wa mshambuliaji huyo ndani na nje ya uwanja. Taarifa hizo zinadai kuwa Benatia alikasirishwa na Greenwood kupuuza majukumu ya kibiashara msimu uliopita wa kiangazi bila kujali madhara yake.