Mason Greenwood aidengulia Jamaica
Muktasari:
- Kocha mkuu wa Jamaica, Steve McClaren alikuwa na matamaoni ya kumjumuisha mshambuliaji huyo wa Marseille katika kikosi chake kwa ajili ya mechi za kufuzu Kombe la Dunia dhidi ya Bermuda Ijumaa na Trinidad na Tobago Jumatano.
MARSEILLE, UFARANSA: STAA wa Marseille, Mason Greenwood ameamua kutojiunga na timu ya taifa ya Jamaica kwa sababu bado ana matumaini ya kuichezea timu ya taifa ya England licha ya kupewa uraia na pasipoti mpya.
Kocha mkuu wa Jamaica, Steve McClaren alikuwa na matamaoni ya kumjumuisha mshambuliaji huyo wa Marseille katika kikosi chake kwa ajili ya mechi za kufuzu Kombe la Dunia dhidi ya Bermuda Ijumaa na Trinidad na Tobago Jumatano.
Hata hivyo, Greenwood ambaye kwa sasa ana uraia pacha wa England na Jamaica ambao alipewa miezi kadhaa iliyopita, hadi sasa hajasaini barua ambayo itaidhinisha mabadiliko yake ya kuitumikia rasmi timu ya taifa ya Jamaica.
Kutosaini kwa barua hiyo kunamfanya kuwa na uwezekano wa kucheza England, nchi ambayo alipata nafasi ya kucheza kikosi cha wakubwa Septemba 2020 na alitokea benchi mchezo wa Uefa Nations League dhidi ya Iceland kabla ya kuondolewa kambini pamoja na Phil Foden baada ya kuvunja sheria za Corona na tangu wakati huo hajacheza tena katika timu hiyo.
Kocha McClaren alikiri alihuzunishwa sana na msimamo wa Greenwood, ingawa bado ana matumaini mshambuliaji huyo atakubali kucheza katika taifa hilo mwishoni mwa mwaka.
“Tumempa pasipoti na tulitarajia angekuwa na sisi hapa, lakini katika mazungumzo tuliyofanya na familia yake, wametuambia hajaamua kucheza timu yoyote ya taifa kwa wakati huu,” alisema McClaren.
“Ni huzuni kidogo, labda tutalazimika kuwa na subira zaidi. Tutaendelea kumshawishi kwa sababu najua kutoka kwenye mazungumzo yangu na yake anataka kuichezea Jamaica.”
Greenwood ana sifa ya kuiwakilisha Jamaica kupitia babu yake na anakidhi vigezo vya FIFA kutokana na mabadiliko kwani amecheza chini ya mechi tatu za mashindano rasmi akiwa na England kabla ya kufikisha umri wa miaka 21.
Kiwango alichoonyesha akiwa na klabu ndiyo kimelivutia zaidi benchi la ufundi la timu ya taifa ya Jamaica na msimu uliopita alifunga mabao 21 na kutoa pasi sita za mabao katika Ligi Kuu Ufaransa.