Gordon kutibua utawala wa Yamal Barca
Muktasari:
- Chumba cha kubadilishia nguo cha Barcelona kimepata mtaalamu mwingine wa penalti, Anthony Gordon ambaye akiwa na timu ya taifa ya England Jumatano iliyopita alionyesha tena umahiri wake wa kupiga penalti kwa mafanikio akithibitisha kuwa ni mmoja wa wapigaji bora.
BARCELONA, HISPANIA: LAMINE Yamal alikuwa mchezaji wa Barcelona aliyepiga penalti nyingi zaidi katika msimu wa 2025-26, ambapo alifanya hivyo mara saba katika mashindano yote, ikiwa ni mbili zaidi ya Raphinha. Hata hivyo, kuelekea msimu ujao amepata mshindani mpya na mwenye uwezo mkubwa wa kupiga mikwaju hiyo.
Chumba cha kubadilishia nguo cha Barcelona kimepata mtaalamu mwingine wa penalti, Anthony Gordon ambaye akiwa na timu ya taifa ya England Jumatano iliyopita alionyesha tena umahiri wake wa kupiga penalti kwa mafanikio akithibitisha kuwa ni mmoja wa wapigaji bora.
Lamine alipiga penalti saba katika mashindano yote msimu uliopita (nne katika LaLiga na tatu Ligi ya Mabingwa Ulaya) akifunga sita. Penalti pekee aliyokosa ilikuwa dhidi ya Girona katika LaLiga.
Kwa upande mwingine, Raphinha alipiga penalti tano na kufunga zote, huku Robert Lewandowski akipiga tatu lakini akakosa mbili. Lewandowski hatakuwepo msimu ujao kwa kuwa ameshaondoka baada ya msimu kumalizika, na Lamine anatarajiwa kuendelea kuwa mpigaji mkuu wa penalti wa Barcelona, licha ya kwamba sasa atakuwa na ushindani mkubwa kutoka kwa Gordon.
Gordon ambaye anatajwa kuwa usajili wa kwanza wa Barcelona kwa msimu ujao, ana rekodi bora ya penalti. Katika msimu wa 2025-26 alipiga penalti 10 na kufunga zote, akimaliza msimu akiwa na asilimia 100 ya mafanikio.
Kati ya penalti hizo, tisa alizifunga akiwa na Newcastle United (tatu Ligi Kuu England, tano Ligi ya Mabingwa Ulaya na moja FA), huku moja akiifunga akiwa na timu ya taifa ya England katika mchezo wa kirafiki dhidi ya Costa Rica.
Kwa kawaida, Harry Kane ndiye mpigaji mkuu wa penalti wa England, lakini baada ya kutolewa uwanjani katika mchezo huo, Gordon alichukua jukumu hilo na kulitimiza kwa mafanikio.
Gordon mwenye umri wa miaka 25 anatarajiwa kuimarisha safu ya ushambuliaji ya Barcelona chini ya kocha Hansi Flick. Nafasi yake ya kawaida ni winga wa kushoto, jambo ambalo litamletea ushindani mkubwa Raphinha, lakini pia ana uwezo wa kucheza kama mshambuliaji wa kati au upande mwingine wa ushambuliaji. Hivyo, Yamal hatakuwa na ushindani wa penalti pekee, bali pia atakuwa na msaada mkubwa katika safu ya ushambuliaji ya Barcelona.