Girona, Barca ni vita ya pesa na heshima

Muktasari:

  • Ukiondoa ubingwa ambao Real Madrid imeshauchukua, wapinzani wao wanapambana kuhakikisha wanamaliza walau nafasi ya pili ikiwa ni eneo ambalo zinachuana vizuri Girona na Barcelona.

BARCELONA, HISPANIA: KWA mujibu wa msimamo kila timu katika Ligi Kuu Hispania (La Liga) imebakisha mechi nne kabla ya kufunga hesabu na kumalizika msimu ambapo Real Madrid ndio imeibuka bingwa.

Ukiondoa ubingwa ambao Real Madrid imeshauchukua, wapinzani wao wanapambana kuhakikisha wanamaliza walau nafasi ya pili ikiwa ni eneo ambalo zinachuana vizuri Girona na Barcelona.

Hadi sasa tofauti ya alama baina ya timu hizo ni moja pekee, Barcelona ikiwa na 73 huku Girona ikiwa nazzo 74 ilhali zote zikiwa zimeshacheza mechi 34 na kubakisha mechi nne. Timu hizo zimeshafuzu kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya, hivyo hazipambanii tena kumaliza katika nafasi nne za juu, bali kuna mambo mengine zinayopambania.

Kwanza kabisa zina vita ya pesa. Kawaida utaratibu wa La Liga wa kugawa fedha za haki ya matangazo ya televisheni kwa timu shiriki za ligi hiyo huwa ni nusu ya fedha kugawiwa kwa wote, kisha robo ya nusu iliyobaki inatolewa kwa kuzingatia mechi zilizoonyeshwa za timu husika na robo inayobaki inagawiwa kwa mujibu wa nafasi ambayo timu imemaliza katika msimamo.

Hapa mwisho ndiko pana vita kwa sababu timu inayomaliza nafasi yapili hupata asilimia 15 ya mgawo kisha ile ya tatu hupata asilimia 13. Kwa mujibu wa tovuti ya AS, zile timu nane za juu kila nafasi ina utofauti wa Euro 7 milioni.

Hivyo Barca inataka kupambana kuhakikisha inakunja pesa hizo kwa sababu hali yao ya kiuchumi kwa sasa sio nzuri wakati Girona nayo inapambana pia kuzipata pesa hizo.

Huu ni msimu wa nne kwa Girona kushiriki La Liga mara ya kwanza ikiwa ni 2017-18, timu hii imeanzishwa mwaka 1930 na hivi karibuni imepata nguvu ya kutosha baada ya  City Football Group kuwa mmiliki wao ikiwa na hisa 47.

City Football Group ndio kampuni inayoimiliki Manchester City chini ya tajiri wao Sheikh Mansoor.

Kwa udogo wao ukilinganisha na Barca ambayo ina historia ya kutosha na ndio walikuwa mabingwa wa msimu uliopita itakuwa ni jambo la aibu kwa vigogo hao ikiwa watavukwa na Girona.

Licha ya ukweli kwamba wameshindwa kutetea taji lao, mashabiki wa Barca watajisikia vibaya zaidi kama wakishindwa kumaliza hata nafasi ya pili.

Mbali ya heshima ambayo Barca inapambana kuilinda kutokana na udogo wa Girona pia kuna hili lingine la eneo ambalo timu hii inatokea.

Timu hizi zote zinatokea Catalona, eneo ambalo mara kadhaa lilidaiwa kuhitaji uhuru wao kutoka kwa Hispania.

Girona inatoka Kaskazini Mashariki mwa Catalona ambako panaonekana kuwa ni vijijini wakati Barcelona Mjini.

Mara nyingi wakazi wa Girona ambako kuna watu takriban 100,000 wanaonekana kama ‘washamba’ na hawaendi na usasa ukilinganisha na wale wa Barcelona ambako ndio katikati ya Mji. Hivyo inafanya kila shabiki wa timu hizi mbili kutaka kutamba kwa timu yake kumaliza juu ya nyingine kudhihirisha ubabe.