Ghafla Casemiro kapindua meza

Muktasari:
- Staa huyo wa zamani wa Real Madrid alionekana kabisa angeachana na miamba hiyo ya Old Trafford dirisha lijalo la uhamisho wa majira ya kiangazi kutokana kushuka sana kiwango uwanjani.
MANCHESTER, ENGLAND: KIUNGO wa Kibrazili, Casemiro huenda akacheza na kumalizia maisha yake ya kisoka kwenye kikosi cha Manchester United baada ya kurudi kwenye kiwango bora kabisa chini ya Kocha Ruben Amorim.
Staa huyo wa zamani wa Real Madrid alionekana kabisa angeachana na miamba hiyo ya Old Trafford dirisha lijalo la uhamisho wa majira ya kiangazi kutokana kushuka sana kiwango uwanjani.
Lakini, kiungo huyo ameonekana akiwa kwenye kiwango bora kabisa wiki za karibuni hasa kwenye michuano ya Europa League, ambako Man United imetinga fainali.
Taarifa za kutoka ndani ya Man United zinafichua kwamba kocha Amorim amekuwa akifanya kazi kwa karibu sana na kiungo huyo kwenye uwanja wa mazoezi huko Carrington, ambapo kwa sasa inaonekana Mbrazili huyo amekuwa mtu muhimu kwenye kuijenga upya klabu hiyo.
Kocha Amorim anaamini uzoefu wa mchezaji huyo na uwezo wa kucheza nafasi tofauti ndani ya uwanja ni silaha kubwa kuwa nayo hasa katika kipindi hiki anachotaka kuipa mafanikio timu hiyo.
Hiyo ina maana kubaki Man United ni suala muhimu kwa Casemiro, ambaye alikuwa akihusishwa na timu za Marekani na Saudi Pro League. Licha ya kwamba akihama atakwenda kupiga pesa nyingi huko, lakini kinachoelezwa ni Casemiro ana furaha kubaki England.
Kwa sasa analipwa Pauni 375,000 kwa wiki, akiwa mmoja wa wachezaji wanaolipwa vizuri kwenye Ligi Kuu England. Casemiro ni bingwa mara tano wa Ligi ya Mabingwa Ulaya.