Fulham yazifuata West Brom, Sheffield

LONDON, ENGLAND. BAADA ya mbio za muda mrefu hatimaye, timu tatu zilizoshuka daraja ndani ya Ligi Kuu England zimejulikana ambapo Fulham ndio ilikuwa ya mwisho kuzifuata West Brom na Sheffield United zilizojikatia tiketi ya Championship mapema.
Fulham iliiaga rasmi Ligi Kuu England baada ya kukubali kichapo cha mabao  2-0 kutoka kwa Burnley iliyokuwa  inajaribu kupambana kusogea nafasi za juu zaidi kwenye msimamo.
Mabishoo hao wa London wameshuka daraja kimahesabu kwani hadi sasa imecheza mechi 35 na imebakisha mechi tatu kabla ya kumaliza ligi na kwenye mechi hizo tatu hata ikishinda zote itakuwa imekusanya alama tisa ambazo ikijumlisha na zile ilizonazo kwa sasa itafikisha 36.
Timu iliyo juu yake kwenye nafasi ya 17 ni Southampton yenye alama 37, hivyo haitaweza kuifikia hata kama Southampton itafungwa mechi zake tatu zilizobaki.
Fulham ilipanda daraja msimu huu baada ya kukosekana kwa muda mrefu na imeshindwa kuhimili vishindo mwisho imeshuka tena.
Ligi hiyo inatarajiwa kuendelea tena leo kwa michezo miwili kupigwa na ule wa mapema zaidi utazikutanisha Manchester United itakayokuwa nyumbani kuialika Leicester City saa 2:00 usiku na Southampton wakiwa kwenye dimba lao la St. Mary's watakuwa wenyeji wa Crystal Palace saa 4:15 usiku.