FIFA yamfungia staa ES Tunis kwa utapeli wa Sh1 bilioni
Muktasari:
- Kwa mujibu wa taarifa, kiungo huyo anayeichezea Espérance Sportive de Tunis kwa sasa, pia ametozwa faini ya faranga za Uswisi 5,000 (Sh14.5 milioni).
SHIRIKISHO la Soka la Kimataifa (FIFA) limemfungia mchezaji wa kimataifa wa Algeria, Youcef Belaïli, kutojihusisha na soka kwa muda wa mwaka mmoja kufuatia mgogoro wa kisheria na klabu yake ya zamani, AC Ajaccio ya Ufaransa.
Kwa mujibu wa taarifa, kiungo huyo anayeichezea Espérance Sportive de Tunis kwa sasa, pia ametozwa faini ya faranga za Uswisi 5,000 (Sh14.5 milioni).
Uamuzi wa FIFA unatokana na madai ya matumizi ya nyaraka za kughushi wakati wa kesi ya madai ya kifedha dhidi ya AC Ajaccio. Mgogoro huo ulianza msimu wa 2022–2023, ambapo AC Ajaccio ilimtuhumu Belaïli kwa kuwasilisha stakabadhi zenye mashaka ili kujaribu kupata malipo ya takriban Euro 380,000 (Sh1 bilioni) kama bonasi na malimbikizo ya mikataba.
Klabu hiyo ya Corsica iliwasilisha shauri FIFA ikidai kufanyiwa jaribio la utapeli, jambo lililopelekea uchunguzi wa miezi kadhaa kabla ya kutoa hukumu hiyo ya mwaka mmoja.
Adhabu hii imekuja wakati mgumu kwa Belaïli ambaye kwa sasa anauguza jeraha la goti lililomweka nje ya uwanja huku akipambana kurejea katika timu ya taifa ya Algeria kwa ajili ya maandalizi ya Kombe la Dunia la 2026.
Belaïli amearifiwa rasmi kuhusu uamuzi huo jana Alhamisi, Machi 5, 2026, na ana nafasi ya kukata rufaa katika Mahakama ya Usuluhishi wa Michezo (CAS) kupinga adhabu hiyo.