Arsenal hakuna namna unaambiwa

Muktasari:
- Kama Arsenal itapindua meza dhidi ya Paris Saint Germain na kutinga fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya utaonekana kuwa ni mwaka wa kibabe kabisa kwa kocha Arteta. Lakini, kama Arsenal itatupwa nje ya michuano, msimu huu utaonekana kuwa wa ovyo kwa miamba hiyo ya Emirates.
LONDON, ENGLAND: LIGI ya Mabingwa Ulaya ni kitu kilichobeba maana kubwa kwenye msimu wa Arsenal. Na hiyo, ndiyo maana usiku wa Jumatano utakuwa wa hukumu kubwa kwa Kocha Mikel Arteta huko Parc des Princes.
Kama Arsenal itapindua meza dhidi ya Paris Saint Germain na kutinga fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya utaonekana kuwa ni mwaka wa kibabe kabisa kwa kocha Arteta. Lakini, kama Arsenal itatupwa nje ya michuano, msimu huu utaonekana kuwa wa ovyo kwa miamba hiyo ya Emirates.
Arsenal ina kazi ngumu ya kufanya baada ya kupoteza mechi ya kwanza kwa bao la Ousmane Dembele. Thomas Partey anarejea kwenye kikosi, lakini PSG imekuwa timu ngumu sana msimu huu itapocheza nyumbani. Kazi ipo.
Arsenal matumaini makubwa yaliyobaki kwenye msimu huu ni Ligi ya Mabingwa Ulaya hasa baada ya kushindwa kwenye vita ya ubingwa wa Ligi Kuu England, huku ikitupwa nje pia kwenye makombe mengine ya ndani na sasa kumeibuka wasiwasi, huenda ikaondoshwa pia kwenye nafasi ya pili kwenye msimamo wa Ligi Kuu England.
Kutokana na hilo, Arsenal itakwenda kufanya mabadiliko makubwa sana kwenye dirisha lijalo la uhamisho wa majira ya kiangazi, ambapo kocha Arteta atalazimika kufanya kazi bega kwa bega na mkurugenzi mpya wa michezo, Andrea Berta - ambaye kwenye meza yake kuna orodha ya mastaa kibao, huku mpango ukiwa ni kufanya usajili wa mastaa wakubwa wasiopungua watatu.
Kinachoaminika huko Emirates ni tayari imeshafanikiwa kunasa saini ya kiungo wa Real Sociedad, Martin Zubimendi na kiungo huyo wa Pauni 51 milioni anajiandaa kutua Emirates.
Arsenal imeweka kwenye mpango wake kuwa Namba 9 ni chaguo kubwa linalofukuziwa kwenye timu hiyo na kwenye hilo orodha ya mastraika kibao wamewekwa ubao, ikiwamo straika wa Sporting Lisbon, Viktor Gyökeres na wa RB Leipzig, Benjamin Sesko sambamba na mkali wa Newcastle United, Alexander Isak.
Arsenal inamtaka pia winga wa kushoto wa Athletic Bilbao, Nico Williams ikimweka kwenye mipango yake, lakini sambamba na hilo itafungua milango ya kuwaondoa Oleksandr Zinchenko, Jorginho na Kieran Tierney huku ikimtaka pia kipa wa Espanyol, Joan Garcia kwenye kuwa chaguo la pili.
Arsenal inatambua wazi kikosi chake kinahitaji maboresho makubwa na kuleta wachezaji wengi wenye uwezo mkubwa ili kuwa na ubora mkubwa hata inapotokea matukio kama ya wachezaji muhimu Bukayo Saka, Gabriel na Kai Havertz kuwa majeruhi.