Fadlu apewa mkono wa kwaheri Raja Casablanca
Muktasari:
- Uamuzi wa kuachana na Fadlu umetolewa siku tatu baada ya Raja kupoteza mechi ya Ligi Kuu Morocco ‘Botola’ dhidi ya Kawkab Marrakech kwa mabao 2-0.
Raja Casablanca imetangaza kuachana rasmi na Kocha wa zamani wa Simba, Fadlu Davids usiku wa kuamkia leo, Juni 12, 2026.
Uamuzi wa kuachana na Fadlu umetolewa siku tatu baada ya Raja kupoteza mechi ya Ligi Kuu Morocco ‘Botola’ dhidi ya Kawkab Marrakech kwa mabao 2-0.
Matokeo hayo yameiporomosha timu hiyo hadi nafasi ya tano kwenye msimamo wa ligi kutoka nafasi ya pili ilipokuwa awali.
Taarifa ya Raja Casablanca imeeleza kwamba mkataba baina yao na Fadlu umevunjwa kwa vile ameshindwa kuendana na matarajio ya klabu hiyo.
“Klabu ya Raja Club Athletic inatangaza kufungwa kwa ushirikiano wake na kocha, Fadluraghman Davids, pamoja na benchi lake la ufundi, kwa makubaliano ya kirafiki kati ya pande zote mbili.
“Klabu inamshukuru Bw. Fadluraghman Davids kwa kipindi chake cha kazi na kikosi cha wakubwa na inamtakia yeye pamoja na benchi lake la ufundi mafanikio mema katika hatua zao zijazo za kitaaluma.
“Aidha, Klabu ya Raja Sports inaendelea kuthibitisha dhamira yake thabiti ya kufanya kazi kwa kujitolea ili kutimiza matarajio ya mashabiki wake waaminifu na kufikia malengo yaliyowekwa, kwa ajili ya kuendeleza hadhi, mafanikio na historia yake kubwa,” imesema taarifa ya Raja.
Fadlu anaachana na Raja Casablanca baada ya kuiongoza kwa miezi tisa tangu alipojiunga nayo, Septemba mwaka jana akitokea Simba.
Fadlu ameiongoza Raja Casablanca katika mechi 23 za Ligi Kuu ya Morocco ambapo timu hiyo imepata ushindi mara 12, imetoka sare sita na kupoteza michezo mitano.