Everton yavunja rekodi

LIVERPOOL, ENGLAND. BAADA ya ukame wa muda mrefu na rekodi mbovu ya kutopata ushindi katika dimba la Anfield tangu 1999, hapo jana Everton ilivunja ukimya na kuitandika Liverpool mabao 2-0 kwenye dimba hilo katika muendelezo wa Ligi Kuu England.
Everton iliandika bao la kwanza mapema katika dakika ya tatu kupitia Richarlison pasi ikitoka kwa James Rodrigue.
Muuaji aliyeitoa nishai Tottenham kwenye mchezo uliopita ndio alishindilia msumari wa pili dakika ya 83 kwa mkwaju wa penalti.
Mbali ya kushinda kwa mara ya kwanza katika dimba la Anfield, Everton pia iliweka rekodi ya kuifunga Liver kwa mara ya kwanza baada ya michezo 24 kupita.
Kwenye mechi hizo 24 za michuano yote, 12 zilimalizika kwa sare na 11 Everton iliambulia kichapo.
Baada ya mchezo huo Everton imepanda hadi nafasi ya saba ikifikisha alama 40 na kuishusha Aston Villa, huku Liverpool ikiendelea kusalia nafasi ya sita ikiwa na alama hizo hizo 40.
Mchezo wa mapema uliopigwa jana katika muendelezo wa ligi hiyo ilikua kati ya Southampton na Chelsea uliomalizika kwa sare ya bao 1-1.
Burnley ikiwa nyumbani nayo ikatoka sare ya 0-0 mbele ya West Brom na ule wa usiku sana ulikua kati ya Fulham na Sheffield iliyolala kwa bao 1-0.