Eti Solskjaer hamjulii Pogba

Thursday November 19 2020
pogba pic

PARIS, UFARANSA. KOCHA wa Ufaransa, Didier Deschamps amezidi kuchochea moto kuhusu hatima ya kiungo, Paul Pogba na maisha yake kwenye kikosi cha Manchester United.

Kocha huyo wa Les Bleus alisema kocha Ole Gunnar Solskjaer hajui namna ya kumtumia Pogba na ndiyo maana Man United haipata fursa ya kushuhudia huduma bora kutoka kwa supastaa huyo.

Pogba aliweka wazi hivi karibuni kwamba maisha yake yamekuwa magumu sana katika kikosi cha Man United. Jambo hilo limeibua uvumi tena wa kumhusisha Mfaransa huyo na mpango wa kuondoka baada ya kusema anapokuwa kwenye timu ya taifa ya Ufaransa ndio anaona kama anavuta hewa safi, jambo linalodaiwa kwamba pengine anaweka sawa mazingira ya kuhama.

Pogba aliisaidia Ufaransa kufuzu kucheza fainali za Nations League mwakani baada ya kuzichapa Ureno na Sweden siku chache zilizopita. Na kocha wa Ufaransa, Deschamps, alimsifu kiungo huyo akisema ni shupaji na mwenye kipaji.

“Jaribu kutazama tu kile alichokifanya dhidi ya Ureno na usiku dhidi ya Sweden,” alisema Deschamps. “Namfahamu vizuri, nafahamu uchezaji wake. Ni jasiri na zaidi ya yote ana kipaji. Unapoamua kukaba, anakaba. Anapokuwa na nafasi ya kuonyesha uwezo wake, anapewa uhuru wa kufanya hivyo.” Pogba mwenyewe alisema yupo kwenye wakati mgumu kwelikweli katika msimu wake huko Man United, aliposema: “Sijawahi kuwa kwenye kipindi kigumu hivi katika maisha yangu ya mpira.”

Advertisement