Endrick apiganiwa England, Madrid yashikilia hatima
Muktasari:
- Klabu hizo za England zinaendelea kufuatilia maendeleo yake kabla ya kuchukua hatua ikiwamo kutuma ofa kwa ajili ya kumsajili katika dirisha lijalo.
TOTTENHAM, Leeds United na Sunderland ni miongoni mwa klabu zinazomfuatilia kwa karibu mshambuliaji chipukizi wa Real Madrid na timu ya taifa ya Brazil, Endrick Felipe, 19, ambaye kwa sasa anang’ara akiwa kwa mkopo Olympique Lyon ya Ufaransa.
Endrick alitolewa kwa mkopo kwenda Lyon ili apate muda mwingi zaidi wa kucheza tofauti na ilivyokuwa Madrid.
Klabu hizo za England zinaendelea kufuatilia maendeleo yake kabla ya kuchukua hatua ikiwamo kutuma ofa kwa ajili ya kumsajili katika dirisha lijalo.
Akiwa na Lyon msimu huu amecheza mechi saba za michuano yote, amefunga mabao manne na kutoa asisti moja.
Hatima ya nyota huyo itategemea msimamo wa Real Madrid baada ya msimu huu kumalizika ingawa inaaminika itakuwa ngumu kwa sababu Real Madrid wanamchukulia kama hazina ya baadae na hawapo tayari kumwachia kirahisi.
Mkataba wake wa sasa unatarajiwa kumalizika 2030. Timu zinazomhitaji zipo tayari kutoa Pauni 40 milioni.
Beto
JUVENTUS imefanya mawasilano ya awali kuhusu uwezekano wa kumsajili mshambuliaji wa Everton, Norberto Bercique Gomes Betunca maarufu Beto, 28.
Hata hivyo, Everton hawapo tayari kumwachia kwa sasa kutokana na ukweli ni mmoja wa washambuliaji wao tegemeo kikosi cha kwanza. Mkataba wake wa sasa unatarajiwa kumalizika 2027.
Dili hilo halionekani kuwa na uwezekano wa kukamilika lakini mambo yanaweza yakawa mazuri dirisha lijalo.
Pablo Garcia
BOURNEMOUTH na West Ham United zimeingia katika vita kali kwa ajili ya kuiwania saini ya winga chipukizi wa Real Betis na timu ya taifa ya Hispania, Pablo Garcia, 19.
Klabu hizo mbili za EPL zipo tayari kulipa kipengele cha kuvunja mkataba cha Pauni 26 milioni ili kumnunua mchezaji huyo ambaye ameonyesha pia kutaka kuondoka baada ya timu hizo za England akiamini ataenda kupata soka la kiushindani zaidi pia kucheza katika ligi hiyo ni moja kati ya ndoto zake. Mkataba wake unatarajiwa kumalizika 2029.
Marcus Rashford
MANCHESTER United haitaweza kuzuia mshambuliaji wao wa kimataifa wa England, Marcus Rashford, 28, kubaki Barcelona ikiwa klabu hiyo ya Hispania itawasilisha ofa ya Euro 30 milioni, kwa mujibu wa masharti ya mkataba wake wa mkopo.
Makubaliano ya mkopo yana kipengele kinachoruhusu Barcelona kumnunua moja kwa moja kwa dau hilo yanampa nguvu staa huyo ikiwa atahitaji kubaki na Barca.
Davide Frattesi
NOTTINGHAM Forest iliachana na mpango wa kumsajili kiungo wa Inter Milan na timu ya taifa ya Italia, Davide Frattesi, 26, siku moja kabla ya dirisha la usajili kufungwa baada ya kuona kuna ugumu kuipata huduma yake.
Inter haikuonyesha nia ya kumwachia Frattesi licha ya kutokuwa mchezaji wao tegemeo kikosi cha kwanza. Forest ilikuwa inapambana kuhakikisha inajenga safu yao ya kiungo baada ya kuanza msimu vibaya.
Arne Engels
CELTIC imekataa ofa ya Pauni 14 milioni kutoka Nottingham Forest kwa ajili ya kumsajili kiungo wa kimataifa wa Ubelgiji, Arne Engels, 22. Celtic inaamini Engels ana mchango mkubwa katika kikosi chao na hawako tayari kumwachia kwa dau dogo.
Mkataba wa sasa wa Engels unatarajiwa kumalizika mwaka 2028, tangu kuanza kwa msimu huu amecheza mechi 38 za michuano yote na kufunga mabao matano.
Denzel Dumfries
LIVERPOOL imeonyesha nia ya kumsajili beki wa pembeni wa Inter Milan, Denzel Dumfries, 29, dirisha lijalo la majira ya kiangazi. Dumfries amekuwa mhimili muhimu Inter kutokana na nguvu, kasi na uwezo wake wa kusaidia mashambulizi.
Liverpool inapambana kuimarisha safu yao ya ulinzi na wanamwona Dumfries kama chaguo sahihi. Inter Milan inahitaji kiasi kikubwa cha pesa ili kumwachia.
Dominik Szoboszlai
WAWAKILISHI wa kiungo wa Liverpool, Dominik Szoboszlai, 25, wapo katika mazungumzo ya mkataba mpya na Liverpool.
Szoboszlai amekuwa mchezaji muhimu Liverpool tangu ajiunge na klabu hiyo. Mazungumzo yanaendelea ili kufikia makubaliano mapya ya muda mrefu. Liverpool wanataka kumbakisha staa huyo kama sehemu ya mipango yao ya baadaye. Mkataba wake unamalizika 2028.