Diallo ajitia kitanzi Manchester United
Muktasari:
- Amad Diallo ameonyesha furaha yake na kuahidi kuendelea kufanya makubwa katika klabu ya Manchester United baada ya kusaini mkata mpya hadi 2030.
LONDON, ENGLAND: Winga wa Manchester United, Amad Diallo amesaini mkataba mpya wa miaka mitano na nusu, ambao utamweka klabuni hapo hadi Juni 2030.
Diallo (22) raia wa Ivory Coast amekuwa na kiwango bora msimu huu, akifunga mabao sita na kutoa kupiga pasi za mwisho saba huku akishinda tuzo ya Mchezaji Bora wa Mwezi wa klabu hiyo mara mbili.
Diallo alieleza furaha yake kwa kuendelea na safari yake na Manchester United akisema, "Nina fahari kubwa kuendelea kuwa sehemu ya klabu hii. Nimekuwa na matukio ya ajabu tayari, lakini bado kuna mengi yanakuja. Nina malengo makubwa kwenye soka na nataka kuandika historia na Manchester United.”
Tangu ajiunge na United kutoka Atalanta mwaka 2021, Diallo alitolewa kwa mkopo katika vilabu vya Rangers na Sunderland, ambako alienda kupata zaidi uzoefu.
Msimu huu, amekuwa mchezaji wa kikosi cha kwanza chini ya meneja, Rúben Amorim, akitoa mchango muhimu, ikiwa ni pamoja na kufunga bao la ushindi dakika za majeruhi dhidi ya Manchester City na kusawazisha dhidi ya Liverpool.