De Bruyne kwenda Arsenal? Arteta apewa majembe sita ya kutwaa taji la ligi

Muktasari:
- Mashabiki wa Arsenal watahitaji majibu, lakini bila shaka huo ni aina ya usajili ambao unaweza kwenda kufanya mabadiliko makubwa kwenye kikosi hicho cha Emirates na kuwa na nguvu kubwa kwenye vita ya kusaka mataji.
LONDON, ENGLAND: SWALI tamu, je Arsenal itamsajili Kevin De Bruyne na Antony dirisha lijalo la uhamisho wa majira ya kiangazi?
Mashabiki wa Arsenal watahitaji majibu, lakini bila shaka huo ni aina ya usajili ambao unaweza kwenda kufanya mabadiliko makubwa kwenye kikosi hicho cha Emirates na kuwa na nguvu kubwa kwenye vita ya kusaka mataji.
Kuna masupastaa sita watahama timu zao dirisha lijalo la majira ya kiangazi huku watatu wakithibitisha hilo, akiwamo fundi wa mpira wa Manchester City, Kevin De Bruyne.
Kwa Arsenal ambayo inaelekea kumaliza ligi ikiwa kwenye nafasi ya pili kwa msimu wa tatu mfululizo, inapaswa kuwa siriazi kwenye mpango wa kunasa wachezaji hao ili kujiweka kwenye wakati mzuri wa kumaliza ukame wa mataji.
Hii hapa orodha hiyo ya mastaa sita ambao Arsenal kama itanasa saini zao itakwenda kuwa balaa zito msimu ujao kwenye mchakamchaka wa kuwania mataji, hasa taji la Ligi Kuu England.
Antony (Man United)
Kingekuwa kitu cha kushangaza kama Arsenal ingefikiria kunasa huduma ya mchezaji huyo miezi michache iliyopita kutokana na kile alichokuwa akufanya uwanjani huko Manchester United. Lakini, tangu alipoenda kwa mkopo Real Betis dirisha la Januari, Antony amekuwa moto kwelikweli na kuisaidia timu hiyo ya La Liga kufika fainali ya Europa Conference League na itakipiga na Chelsea, Mei 28.
Antony inawezekana hakuwa na maajabu kwenye kikosi cha Man United, lakini anaweza kwenda kufaa kwingine, kitu ambacho Arsenal inaweza kufikiria kunasa huduma yake. Kabla hajawasha moto Betis, Man United ingeweza kukubali hata ada ya Euro 15 milioni ya kumuuza mchezaji huyo, lakini kwa sasa bila ya Euro 40 milioni hujamsajili staa huyo nab ado ni hasara.
Kocha Mikel Arteta au bosi wa usajili Andrea Berta wanaweza kumfikiria winga huyo ili kwenda kuwa msaidizi wa Bukayo Saka kwenye wingi ya kulia.
Kevin De Bruyne (Man City)
Martin Odegaard ameonekana kushuka kiwango msimu huu na kuonekana kuzidiwa sana na mzigo wa kuwa mbunifu wa kutengeneza nafasi za mashambulizi katika kikosi hicho. Usajili wa De Bruyne unaweza kwenda kumpunguzia Odegaard majukumu ya kutengeneza nafasi kwenye kikosi cha Arsenal na kufikia malengo ya ubingwa. Shida inaweza kuwa kwenye mahitaji yake ya mshahara mkubwa na rekodi zake za kuwa majeruhi mara kwa mara, lakini De Bruyne ni mchezaji mwenye uwezo mkubwa wa kwenda kubadili hali ya upepo kwenye kikosi hicho Emirates na kufikia malengo ya kushinda ubingwa. Man City analipwa mshahara wa Pauni 400,000 kwa wiki, hawezi tena kwenda kulipwa mshahara mkubwa wa aina hiyo nje ya Saudi Arabia au Marekani.
Arsenal ikichangamkia huduma ya De Bruyne itakwenda kuwapa faida kubwa kwenye kikosi chao kwa sababu atawekeza akili ya ushindi na ndiyo maana Liverpool imekuwa ikihusishwa na mpango wa kumfukuzia kiungo huyo wa Kibelgiji.
Marcus Rashford (Man United)
Arsenal ilifanya usajili wa kupaniki kwenye dirisha lililopita la majira ya kiangazi wakati ilipomsajili Raheem Sterling kwa mkopo akitokea Chelsea, lakini sasa inaweza kuhamia kwa Marcus Rashford. Kwenye dirisha la majira ya baridi, kocha Arteta angefanikiwa kunasa saini ya mshambuliaji huyo angekwenda kumpa msaada mkubwa baada ya washambuliaji wake wengi akiwamo Kai Havertz kuwa majeruhi. Kukosa mshambuliaji wa kati, kulimfanya kocha Arteta kulazimika kumtumia kiungo Mikel Merino kama straika ili kubaki na Gabriel Martinelli kwenye wingi, huku Bukayo Saka naye alikuwa nje ya uwanja kwa muda mrefu na kuigharimu timu kwa namna moja au nyingine.
Kwa kiwango cha Rashford alichokionyesha huko Aston Villa alikojiunga kwa mkopo kwenye dirisha la Januari, Arsenal inaweza kuchangamkia saini yake kwa sababu si mchezaji ambaye Man United imemweka kwenye mipango yao kwa ajili ya kumrudisha kikosini. Man United inajaribu kuachana na Rashford ili kupunguza makali kwenye bili yao ya mishahara.
Christopher Nkunku (Chelsea)
Nkunku alifunga mabao 58 na kuasisti mara 29 katika misimu yake miwili ya mwisho klabuni RB Leipzig na hivyo kubamba dili la kujiunga Chelsea.
Hata hivyo, makali ya Nkunku tangu alipotua Chelsea hayakuwa ya kiwango kama kile cha RB Leipzig na jambo hilo ndilo linawafanya The Blues kufikiria mpango wa kuachana naye mwishoni mwa msimu huu wakati dirisha la uhamisho wa majira ya kiangazi litakapofunguliwa. Kwa aliyewahi kumwona Nkunku alipokuwa akiwatesa makipa na mabeki kwenye Bundesliga hawezi kupuuzia mpango wa kunasa saini yake, hivyo Arsenal itakuwa imepata mtu wa maana wa kumwongeza kwenye kikosi chao endapo kama itafanikiwa kupata huduma yake.
Evan Ferguson (Brighton)
Straika Evan Ferguson ameonyesha kiwango bora cha soka lake, lakini akiwa chini ya kocha makini anaweza kuwa matata zaidi ndani ya uwanja. Kama Arsenal itafanya uamuzi wa kwenda kunasa saini ya mshambuliaji huyo anaweza kwenda kuwa na faida kubwa kwenye kikosi chao kuliko hata kuhangaikia saini za washambuliaji waliojipata zaidi, Viktor Gyokeres, Benjamin Sesko na Jonathan David. Sawa, Arsenal inaweza kunasa huduma ya straika mmoja wa kiwango cha dunia, lakini bado ikapambana kupaa saini ya Ferguson ili kuwa na kikosi chenye mastraika wakali kwa yule anayeanza na mwingine anayetokea benchini.
Kobbie Mainoo (Man United)
Man United inaripotiwa kuweka ubaoni majina ya mastaa kibao ambao ipo tayari kuwapiga bei kwenye dirisha lijalo la uhamisho wa majira ya kiangazi akiwamo kiungo Kobbie Mainoo, endapo kama kutakuwa na ofa tamu mezani. Man United itamuuza Mainoo kama itaona pesa itakayopata itakuwa ya faida kubwa kwenye mauzo hayo.
Arsenal pia itahitaji kiungo wa kuja kuboresha kikosi chao kwenye safu hiyo wakati itakapoachana na Jorginho. Sawa Martin Zubimendi anaweza kuwasili kwenye timu hiyo katika dirisha lijalo la majira ya kiangazi kwa ada ya Pauni 51 milioni. Na kama Thomas Partey ataamua kuondoka pia kama anavyofanya Jorginho, basi kocha Arteta atakuwa kwenye mikono salama kabisa akifanikiwa kupata huduma ya Mainoo, ambaye ni pesa yake tu. Uzuri wa Mainoo ni anaweza kucheza kama Namba 6, 8 au Namba 10, kitu kitakachompa faida Arteta kwenye machaguo ya upangaji wa kikosi chake kulingana na aina ya mpinzani anayekabiliana naye.