De Bruyne kujiunga timu haijacheza mechi
Muktasari:
- Staa huyo mshindi mara sita wa taji Ligi Kuu England inaelezwa kwamba anaweza kuachana na Manchester City kwenda kujiunga na timu mpya ya Ligi Kuu Marekani, San Diego, ambayo haijacheza mechi yoyote ya soka.
MANCHESTER, ENGLAND: KIUNGO, Kevin De Bruyne inadaiwa kwamba yupo kwenye hatua za mwisho kabisa za kujiunga na timu ambayo haijawahi kucheza mechi hata moja.
Staa huyo mshindi mara sita wa taji Ligi Kuu England inaelezwa kwamba anaweza kuachana na Manchester City kwenda kujiunga na timu mpya ya Ligi Kuu Marekani, San Diego, ambayo haijacheza mechi yoyote ya soka.
Mbelgiji huyo mwenye umri wa miaka 33, alisema wala hana hofu yoyote endapo kama Man City haitampa ofa ya mkataba mpya wakati huu wa sasa unaofika tamati mwishoni mwa msimu huu. Inaelezwa pia, KDB anaweza kuchagua kwenda kujiunga na ligi ya pesa nyingi, Saudi Pro League.
Na sasa kinachoripotiwa ni kwamba San Diego ipo mstari wa mbele kwenye kufukuzia huduma ya kiungo huyo matata kabisa.
De Bruyne amerejea uwanjani kwa sasa kwenye kikosi cha Pep Guardiola na alitoa asisti wakati Man City iliposhinda 4-1 dhidi ya West Ham kwenye Ligi Kuu England, Jumamosi iliyopita, ambapo alicheza kwa dakika zote 90.
Na De Bruyne alisema: “Katika umri kama wangu, unapaswa kukubaliana na kila kitu.”
Na alipoulizwa kuhusu kwenda kujiunga na Cristiano Ronaldo na mastaa wengine huko Saudi Arabia, alisema: “Unazungumzia kiwango kikubwa sana cha pesa na hiyo pengine itakuwa hatua ya mwisho kabisa ya maisha yangu ya soka. Wakati mwingine nafikiria hilo.”
Hata hivyo, ripoti nyingine zinadai, KDB na San Diego wamekuwa kwenye mazungumzo kwa miezi kadhaa na mambo yanaonekana kuiva.
Timu hiyo itaingia kwenye MLS msimu huu kwa upande wa Western Conference, ambapo mechi yao ya kwanza itacheza dhidi ya LA Galaxy, Februari 23.