Dani Carvajal kukaa nje mwezi mzima
Muktasari:
- Inaelezwa jeraha hilo linatarajiwa kumweka nje ya Uwanja kwa takribani mwezi mmoja na hiyo imeifanya Madrid kuwa katika hali ngumu kwani haina hata beki mmoja wa kulia.
MADRID, HISPANIA: REAL Madrid imejikuta katika mgogoro mkubwa wa safu ya ulinzi baada ya beki wao Dani Carvajal kupata jeraha la mguu katika mechi ya dabi dhidi ya Atletico Madrid.
Inaelezwa jeraha hilo linatarajiwa kumweka nje ya Uwanja kwa takribani mwezi mmoja na hiyo imeifanya Madrid kuwa katika hali ngumu kwani haina hata beki mmoja wa kulia.
Trent Alexander-Arnold ambaye ndiye aliyekuwa akiwania namba na Carvajal naye ana majeraha ambayo yatamweka nje kwa muda wa wiki nane.
Madrid ilitoa taarifa Jumapili ya wiki iliyopita kapteni wao Carvajal, 32, alipata jeraha la misuli ya mguu wake wa kulia katika mechi dhidi ya Atletico Madrid na atakosekana kwa wiki nne.
Awali Madrid iliona kuna shida eneo hilo kiasi cha kuamua kumsajili Trent lakini sasa mambo yamekuwa ni yaleyale.
Kwa sasa inaweza ikamchezesha Federico Valverde katika eneo hilo au nyota Raul Asencio ingawa ufanisi wao ni tofauti na ilivyokuwa kwa Carvajal mwenyewe au Trent ambao ni eneo lao la kiasili.
Kukosekana kwa Carvajal na Trent imekuwa pigo kubwa sana kwa Madrid kwani ina muda mchache kabla ya kucheza na wapinzani wa karibu Barcelona, Oktoba 26 na kuna asilimia nyingi yeye na Trent kutokuwa tayari kucheza kwa wakati huo.
Hali kama hii iliwahi kutoka Januari mwaka huu katika mechi ya Ligi ya Mabingwa Ulaya Madrid ililazimika kumchezesha Valverde kama beki wa kulia.