DAH! Nico aiambia Bilbao ‘Naondoka’

Muktasari:
- Staa huyo anatarajia kusababisha vita kali kwenye msako wa kunasa saini yake baada ya kuonyesha kiwango bora akiwa na timu yake ya Bilbao na timu ya taifa.
MADRID, HISPANIA: WINGA Mhispaniola, Nico Williams ameiambia klabu yake ya Athletic Bilbao kwamba anataka kuhama kwenda kujiunga na Barcelona kwenye dirisha hili la uhamisho wa majira ya kiangazi.
Staa huyo anatarajia kusababisha vita kali kwenye msako wa kunasa saini yake baada ya kuonyesha kiwango bora akiwa na timu yake ya Bilbao na timu ya taifa.
Arsenal inamtazama kama mchezaji muhimu wa kuingia kwenye mipango yao kwa ajili ya msimu ujao ili akacheze wingi ya kushoto ili kuongeza makali kwenye fowadi ya kikosi hicho cha kocha Mikel Arteta. Lakini, mpango huo wa Arsenal wa kumsaka fowadi huyo mwenye umri wa miaka 22 unaweza kuishia kwenye masikitiko makubwa kutokana na anachotaka mchezaji.
Barcelona sasa ipo bayana kabisa inahitaji saini ya Williams kutoka kwa wapinzani wao hao wa La Liga, ambapo winga huyo mwenyewe huenda akalazimisha dili la kutua Catalunya.
Ripoti zinafichua Williams ameiambia klabu ya Bilbao kwamba anataka kuachana na timu hiyo kwenda kujiunga na wapinzani wao kwenye La Liga.
Williams aliripotiwa kufikia makubaliano binafsi na Barcelona na sasa kinachosubiriwa ni Barcelona kulipa Euro 60 milioni ili kuvunja mkataba wa winga huyo kama kinavyobainisha kipengele kilichowekwa kwenye mkataba wake. Hata hivyo, dili hilo litaanza kufanyiwa kazi Julai ili kupisha kipindi cha kuwasilisha hesabu za kifedha za mwaka.
Lakini, Barcelona bado inahitaji kujihakikishia uwezo wake wa wa kulipa mishahara kwamba isivuke kiwango kwa ajili ya msimu ujao. Na kuhusu dili la Williams, mkurugenzi wa michezo wa Barcelona, Deco alisema: “Tunahitaji kuboresha nguvu kwenye eneo hili. Kwa mawinga, tunao Lamine (Yamal) na Raphinha. Kuanzia hapo, kuna watu wataondoka na tutaangalia ishu ya gharama na viwango.” Williams alifunga mabao 11 na asisti saba Bilbao msimu uliopita.