Kompany alivyomaliza gundu la Harry Kane

Muktasari:
- Na sasa, Kane hana gundu tena. Ni bahati mbaya tu alikuwa akicheza kwenye klabu iliyoshindwa kumpa fursa hiyo ya kushinda ubingwa na alitua Bayern ikiwa kwenye kipindi kigumu na kushindwa kubeba ubingwa msimu uliopita.
MUNICH, UJERUMANI: MAKOCHA kibao walijaribu. Na wote walishindwa. Lakini, Vincent Kompany alifanikiwa kufanya kitu kilichowashinda magwiji kama Mauricio Pochettino, Jose Mourinho, Antonio Conte na Gareth Southgate kushinda taji kubwa ukiwa na Harry Kane kwenye timu baada ya Bayern Munich kunyakua taji la Bundesliga, shukrani kwa sare ya Bayer Leverkusen na Freiburg iliyowafanya Bavaria kuongoza ligi kwa pointi nane kwenye msimamo na ligi imebakiza mechi mbili tu.
Na sasa, Kane hana gundu tena. Ni bahati mbaya tu alikuwa akicheza kwenye klabu iliyoshindwa kumpa fursa hiyo ya kushinda ubingwa na alitua Bayern ikiwa kwenye kipindi kigumu na kushindwa kubeba ubingwa msimu uliopita.
Kulikuwa na maswali mengi kuhusu Bayern kama ingenyakua taji hilo la Bundesliga lililobebwa na Leverkusen msimu uliopita baada ya mabadiliko ya kocha, Thomas Tuchel na kuletwa Kompany, ambaye alikuwa na kibarua cha kuja kushindana na timu ya Xabi Alonso iliyotoka kubeba taji la Bundesliga bila ya kupoteza mchezo wowote.
Kompany, ambaye alikuwa chaguo la kwanza la klabu hiyo amefanikiwa kuirudisha Bayern kwenye mstari.
Uteuzi wake uliibua maswali mengi, lakini Kompany amezima midomo ya watu kwa vitendo kwa kubeba ubingwa wa Bundesliga.
Amefanyaje? Ni kipi amefanya Kompany kutoka kuishusha daraja Burnley kwenye Ligi Kuu England hadi kwenda kunyakua taji la Bundesliga huko Ujerumani kwa muda usiodizi mwaka mmoja? Cheki hapa...

Kutoka Burnley kwenda Bayern
Kompany aliongoza Burnley kurudi kwenye Ligi Kuu England kwa kushinda ubingwa wa Championship msimu wa 2022-23 na baada ya hapo alipata sifa nyingi na kusifiwa staili ya uchezaji ya timu yake.
Hata hivyo, Burnely ilishuka daraja, lakini Kompany aliendelea kushikilia falsafa zake na kumpatia dili la kwenda kuinoa Bayern, siku 10 baada ya Burnley kushuka daraja huko kwenye Ligi Kuu England ikiwa na pointi 24 katika mechi 38.

Bayern imemwaamini
Kilichotokea si kwamba Bayern hakuwa na machaguo mengine ya makocha ambao ingewanasa na kuwapa kazi, lakini iliamini Kompany ni mtu sahihi kwa timu yao kwa kipindi hicho. Alonso, Julian Nagelsmann, Ralf Rangnick na Oliver Glasner waligomea kazi ya kwenda kuinoa timu hiyo baada ya kuona itakuwa shughuli kubwa kufuatia Tuchel ilivyomshinda.
Mkurugenzi wa michezo wa Bayern, Max Eberl, ambaye ni shabiki mkubwa wa Kompany aliamini Mbelgiji huyo ana kitu kikubwa na kwenda kuanzisha zama mpya Allianz Arena.
Chaguo sahihi Bayern
Mwenyekiti wa zamani wa bodi ya Bayern, Karl-Heinz Rummenigge mwanzoni hakushawishika kuhusu uteuzi wa Kompany, asiyekuwa na uzoefu wa kutosha wa kutoa timu kubwa yenye ushindani kwenda kuwa kocha wa klabu yenye hadhi kama Bayern, lakini alikubali baada ya kusikia kauli ya Eberl alizungumza na Pep Guardiola, kocha aliyekuwa na heshima kubwa huko Allianz Arena, ambaye ukiacha ishu ya kushinda mataji matatu mfululizo ya Bundesliga akiwa na Bayern, alimnoa pia Kompany kwa mafanikio makubwa akiwa nahodha wake huko Manchester City.

Bayern imempata Guardiola mpya
Bayern ilianza msimu kwa kuvunja rekodi kibao kwenye Bundesliga msimu huu, kwa kushinda mechi nne mfululizo, huku ikianza msimu wake wa Ligi ya Mabingwa Ulaya kwa ushindi wa mabao 9-2 dhidi ya Dinamo Zagreb.
Kutokana na namna inavyocheza kwa kuhakikisha anakuwa na mpira muda wote, jambo hilo lilimfanya Kompany asifiwe kwa falsafa zake za kiuchezaji ambazo zimemfanya alinganishwe na Guardiola, kwamba Bayern muda wote inataka kuwa na mpira na kuuweka kwenye himaya yake.
Kompany alikuwa akiwataka wachezaji wake waongeze moto wa kushambulia hata kama ni dakika 88 ya mchezo.

Ushirikiano mkubwa kwenye timu
Bayern ilikuwa na vitu vingi vya kufanya kwenye kikosi chake, hasa kwenye safu ya ulinzi ambapo walionyesha eneo hilo linashinda baada ya kukumbana na vipigo kadhaa kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya kama kile cha 4-1 dhidi ya Barcelona na kile kipigo cha kushtua cha mabao 3-0 kutoka kwa Feyenoord.
Lakini, Kompany alibadili makali yake kwenye safu hiyo ya ulinzi. Chini yake, beki ya Bayern ilianza kuwa imara kabisa na kubadili viwango vya Dayot Upamecano na Kim Min-jae waliokuwa wakifanya makosa mengi kubadilika na kuwa wachezaji muhimu sana uwanjani. Kompany alimshawishi hadi Joshua Kimmich, aliyekuwa tayari kuachana na Bayern kukubali kusaini mkataba mpya wa kuendelea kubaki kwenye timu hiyo baada ya kukoshwa na kile kinachofanya na Kompany.

Kompany ameweka viwango
Wachezaji walianza kumwelewa Kompany kwa namna alivyokuwa akiwajenga kisaikolojia baada ya kukumbana na matokeo mabaya uwanjani. Wachezaji waliokuwa wakifanya makosa binafsi uwanjani ambao mwanzoni walikuwa wakikosolewa mbele ya waandishi wa habari, Kompany alikwenda kumaliza matatizo hayo kwenye vyumba vya kubadilishia.
Baada ya hapo, wachezaji wa Bayern waliokuwa wakikosolewa sana hapo awali huo mtindo ulianza kupungua. Kwa maana hiyo, Kompany aliweka utulivu mkubwa kwenye kikosi hicho na kuifanya kucheza kwa ushirikiano mkubwa hata kwenye kipindi ambacho iliwapoteza mastaa wake muhimu kama Upamecano, Kim, Manuel Neuer, Alphonso Davies na Jamal Musiala kutokana na kuwa majeruhi.