Cunha amtaka Zirkzee abaki
Muktasari:
- Zirkzee amekuwa akihusishwa kwa nguvu na uhamisho wa kwenda AS Roma katika dirisha la usajili la Januari, lakini ametoa mchango muhimu kwa Man United katika wiki za hivi karibuni.
MANCHESTER, ENGLAND: STAA, Matheus Cunha amemwambia Joshua Zirkzee kuwa anapaswa kusahau wazo la kuondoka Manchester United na kujikita zaidi katika kusaidia timu.
Zirkzee amekuwa akihusishwa kwa nguvu na uhamisho wa kwenda AS Roma katika dirisha la usajili la Januari, lakini ametoa mchango muhimu kwa Man United katika wiki za hivi karibuni.
Mshambuliaji huyo wa Kidachi mwenye umri wa miaka 24 amepata wakati mgumu tangu alipojiunga na Man United kwa ada ya Pauni 36.5 milioni akitokea Bologna mwaka 2024.
Ameshindwa kujihakikishia nafasi ya kudumu katika kikosi cha kwanza chini ya kocha Ruben Amorim, ambaye mapema Jumatatu alifunguliwa mlango wa kutokea huko Old Trafford.
Hata hivyo, alianza na kufunga bao katika sare ya 1-1 dhidi ya Wolves wiki iliyopita, na alipoingia kutoka benchini aliasisti bao la kusawazisha la Cunha katika sare dhidi ya Leeds siku ya Jumapili.
Kutokuwepo kwa Bryan Mbeumo na Amad waliopo kwenye mashindano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) kumemfanya Zirkzee kuwa mchezaji muhimu zaidi kwa Man United, hali inayotia shaka kuhusu kuondoka kwake.
Mdachi huyo aliripotiwa kukutana na mkurugenzi wa michezo wa Roma, Ricky Massara, na amepewa uhakika na kocha Gian Piero Gasperini kuwa atafaa katika mfumo wa timu hiyo.
Hata hivyo, Cunha amemsihi mwenzake abaki, avumilie hali iliyopo na kusaidia Man United katika kipindi hiki kigumu.
“Josh ni mchezaji mzuri sana,” amesema Cunha.
“Ninahisi ana ubora mkubwa. Bila shaka hali yake si rahisi, lakini ana kila kitu cha kubadilisha hali hiyo. Tunamhitaji. Anahitaji kuelewa hilo, ndipo kila mtu ataweza kumtegemea.”
Zirkzee ameanza mechi nne tu za Ligi Kuu msimu huu kufuatia usajili wa Pauni 200 milioni wa wachezaji Benjamin Sesko, Cunha na Bryan Mbeumo katika dirisha la majira ya kiangazi.