Crouch, Keown wabishana kuhusu Eze wa Arsenal
Muktasari:
- Eze, 27, alitolewa wakati wa mapumziko katika sare ya 1-1 dhidi ya Brentford FC, akishindwa kutumia vizuri nafasi yake. Hiyo ilikuwa mechi yake ya kwanza kuanza katika Ligi Kuu England baada ya miezi miwili.
LONDON, ENGLAND: NOMA sana. Staa, Eberechi Eze ameambiwa kuwa Mikel Arteta “hamkubali sana” kufuatia kikosi hicho kubanwa na Brentford katika mchezo wa Ligi Kuu England uliofanyika Alhamisi iliyopita.
Eze, 27, alitolewa wakati wa mapumziko katika sare ya 1-1 dhidi ya Brentford FC, akishindwa kutumia vizuri nafasi yake. Hiyo ilikuwa mechi yake ya kwanza kuanza katika Ligi Kuu England baada ya miezi miwili.
Mbadala wake, Martin Odegaard, alileta mabadiliko chanya katika uchezaji wa Arsenal ambayo ilipata bao la kuongoza muda mfupi baadaye. Hata hivyo, The Gunners waliruhusu bao la kusawazisha na kulazimika kuridhika na sare ya 1-1.
Uchezaji dhaifu wa Eze ulimletea ukosoaji. Kiungo huyo amekuwa akipata ugumu kuzoea tangu alipojiunga na klabu hiyo kwa ada ya Pauni 67.5 milioni akitokea Crystal Palace, Agosti mwaka jana. Amefunga mabao matano na kutoa asisti mbili.
Akizungumza baada ya mechi, mshambuliaji wa zamani wa Tottenham, Peter Crouch aliiambia TNT Sports: “Ninaamini hakuwa ameanza mechi katika tisa zilizopita au kitu kama hicho, hivyo alipata nafasi na unafikiri, ‘sawa, nenda kajithibitishe’. Kwa bahati mbaya alionekana yuko nje ya kiwango, hakuweza kuupata mpira vizuri kipindi cha kwanza. Ilikuwa ngumu kwa Arsenal kwa ujumla. Nilimuonea huruma. Na hakupi kile ambacho Odegaard anakupa katika presha na pia haathiri mchezo anapokosa mpira. Kwa ukweli, alionekana kama abiria tu. Tuliona baada ya dakika 30 kwamba angeondolewa kwa sababu kwa namna fulani inaonekana kwa sasa Arteta hamkubali sana. Hilo linaweza kuathiri nafasi zake katika timu ya England.”
Hata hivyo, gwiji wa Arsenal, Martin Keown hakukubaliana na Crouch na ana uhakika kuwa Eze atafanikiwa aliposema: “Kusema kuwa hamkubali, nafikiri ni zaidi ya kwamba mchezaji bado hajaielewa vizuri mfumo wa timu kama Odegaard anavyoelewa.”