Cristian Romero aikacha Spurs, atimkia Argentina
Muktasari:
- Nyota huyo wa safu ya ulinzi hakuhudhuria mechi ambayo Spurs ilipoteza dhidi ya Chelsea, Jumanne katika matokeo yaliyoiacha Tottenham ikihitaji pointi moja katika mchezo wa nyumbani dhidi ya Everton ili kujinusuru kushuka daraja kwa mara ya kwanza tangu 1977.
LONDON, ENGLAND: Nahodha wa Tottenham Hotspur, Cristian Romero amezua hofu baada ya kusafiri kwenda nchini kwao Argentina kushuhudia fainali ya klabu yake ya utotoni ya Belgrano, huku Spurs ikikabiliwa na mechi ngumu dhidi ya Everton, Jumapili hii.
Romero mwenye umri wa miaka 28 na mshindi wa Kombe la Dunia 2022, yupo nje ya uwanja baada ya kuumia goti mwezi uliopita. Licha ya jeraha hilo, alikuwa akishirikiana bega kwa bega na kocha mkuu Roberto De Zerbi na wachezaji wenzake, lakini wiki hii ameshtua wengi kwa kuondoka kambini.
Nyota huyo wa safu ya ulinzi hakuhudhuria mechi ambayo Spurs ilipoteza dhidi ya Chelsea, Jumanne katika matokeo yaliyoiacha Tottenham ikihitaji pointi moja katika mchezo wa nyumbani dhidi ya Everton ili kujinusuru kushuka daraja kwa mara ya kwanza tangu 1977.
Kupitia mitandao ya kijamii, Romero amechapisha picha akiwa kwenye ndege binafsi na familia yake, akiipongeza Belgrano inayojiandaa kucheza fainali za ubingwa wa Argentina dhidi ya River Plate huko Cordoba.
Rais wa Belgrano, Luis Artime, amethibitisha kuwa Romero atakuwa sehemu ya wageni rasmi wa klabu hiyo kwenye fainali na amepewa ruhusa ya kutumia vifaa vya mazoezi kwa ajili ya matibabu.
Beki huyo anapambana kuwahi makali ya mwili wake ili kujumuishwa kwenye kikosi cha kocha Lionel Scaloni kwa ajili ya kutetea ubingwa wa Kombe la Dunia 2026 mwezi ujao nchini Marekani, Mexico, na Canada.
Romero alipewa unahodha wa Spurs mwaka jana na aliyekuwa kocha Thomas Frank baada ya kuondoka kwa Son Heung-min. Hata hivyo, tetesi zinasema amekuwa na hamu ya kuondoka klabuni hapo huku akihusishwa na Barcelona, licha ya kusaini mkataba mpya mwezi Agosti unaomfunga klabuni hapo hadi mwaka 2029.
Alipoulizwa kuhusu mustakabali wa nahodha huyo kwa msimu ujao, kocha De Zerbi amesema: "Hilo ni swali zuri lakini muda wake si sahihi. Jambo la muhimu zaidi ni tabia na nia ya mchezaji kutaka kubaki katika klabu hii. Tutafanya uamuzi baada ya msimu huu na baada ya mchezo wa Everton."
Katika hatua nyingine, beki Djed Spence anatarajiwa kuwepo uwanjani siku ya Jumapili dhidi ya Everton licha ya kuvunjika taya katika mchezo dhidi ya Chelsea.
Spence aligongwa usoni na Liam Delap lakini atafanyiwa vipimo na kuvalishwa ‘kinyago maalumu’ cha kinga (protective mask) ili kuisaidia Spurs kupigania pointi moja muhimu.