Coutinho kutua London

Monday September 27 2021
cout pic

LONDON, ENGLAND. MMESIKIA! Kila kitu kipo sawa kuelekea dirisha lijalo la majira ya baridi na kiungo wa Barcelona na Brazil, Philippe Coutinho atatua England kwa sababu Arsenal na Tottenham zipo kwenye mazungumzo na mabosi wa Barca ili kuipata saini yake.

Barca ipo tayari kumuuza Coutinho kwa sababu hali yao ya kiuchumi sio nzuri na mshahara wa staa huyo wa Pauni 200,000 kwa wiki unazidi kuiweka bajeti yao njia panda.

Tangu kuanza kwa msimu huu Coutinho amecheza dakika 82 pekee za michuano yote ikiwa ni baada ya kurejea kutoka kwenye majeraha yaliyokuwa yanamsumbua tangu msimu uliopita.

Coutinho amekuwa hapati nafasi ya kucheza kwenye kikosi cha kwanza tangu atue kwenye viunga hivyo Camp Nou mwaka 2018 kwa dau la Pauni145 milioni lililovunja rekodi ya mauzo kwa upande wa Ligi Kuu England.

Taarifa zinadai mchezaji huyo angependa zaidi kurejea Liverpool lakini wababe hao hawajaonyesha mpango wa kumchukua kiungo huyo wa ushambuliaji aliyewahi kushinda tuzo ya mchezaji bora wa msimu mfululizo kuanzia mwaka 2014 hadi 2016.

Kiungo huyu aliwahi kushinda taji la Ligi ya Mabingwa mwaka 2020 akiwa na Bayern Munich aliyokuwa anaitumikia kwa mkopo na kwenye mchezo wa nusu fainali dhidi ya Barca alifunga mabao mawili.

Advertisement
Advertisement