Conte atangaza kubwaga manyanga Napoli
Muktasari:
- Kocha huyo wa zamani wa Chelsea na Tottenham Hotspur alichukua mikoba ya Napoli mwaka 2024 na katika msimu wake wa kwanza aliiletea klabu hiyo ubingwa wa nne wa ligi kuu katika historia yao.
Turin, Italia: Kocha Antonio Conte ametangaza ataondoka Napoli msimu huu ikiwa ni miezi 12 baada ya kuiongoza klabu hiyo kutwaa ubingwa wa Serie A.
Kocha huyo wa zamani wa Chelsea na Tottenham Hotspur alichukua mikoba ya Napoli mwaka 2024 na katika msimu wake wa kwanza aliiletea klabu hiyo ubingwa wa nne wa ligi kuu katika historia yao.
Hata hivyo, msimu huu Napoli walimaliza nafasi ya pili, wakiwa pointi 11 nyuma ya mabingwa Inter Milan.
Katika mashindano ya Ligi ya Mabingwa ambayo Conte amekuwa akipata ugumu kufanya vizuri Napoli walishindwa kufuzu hatua ya mtoano.
Baada ya Napoli kuifunga Udinese bao 1-0 Jumapili katika mchezo wao wa mwisho wa msimu, Conte alitangaza kuondoka kwake katika mkutano wa pamoja na waandishi wa habari akiwa pamoja na rais wa klabu, Aurelio De Laurentiis.
“Ilikuwa heshima kubwa, ni jambo la kipekee kuifundisha Napoli. Imekuwa misimu miwili mizuri, uzoefu wa kipekee sana,” Conte aliwaambia vyombo vya habari vya Italia.
“Ilikuwa uamuzi wangu, nilimwambia mwenyekiti wiki chache zilizopita. Napoli itabaki kuwa nyumbani kwangu daima.”
Alipoulizwa kama anaweza kuwa kocha mpya wa timu ya taifa ya Italia, Conte alijibu kwa utani:
“Ushauri wangu ungekuwa wamchukue Pep Guardiola.
Conte alionekana kuwa karibu kuondoka klabuni msimu uliopita wa kiangazi, lakini alishawishika kubaki baada ya mazungumzo na De Laurentiis.
Napoli walileta usajili mpya akiwemo Kevin De Bruyne na Rasmus Højlund, lakini majeraha pamoja na kutokuwa na mwendelezo mzuri wa matokeo vilikwamisha jitihada zao za kutetea ubingwa.