Chicago Fire wanamtaka Lewandowski
Muktasari:
- Berhalter alisema mazungumzo na mshambuliaji huyo wa kimataifa wa Poland pamoja na wawakilishi wake yamekuwa yakiendelea kwa muda.
CHICAGO, MAREKANI: KOCHA wa Chicago Fire, Gregg Berhalter amethibitisha kuwa klabu hiyo inamtaka mshambuliaji wa zamani wa Barcelona na Bayern Munich, Robert Lewandowski.
Berhalter alisema mazungumzo na mshambuliaji huyo wa kimataifa wa Poland pamoja na wawakilishi wake yamekuwa yakiendelea kwa muda.
“Ninaweza kuzungumza wazi kwa sababu siyo mchezaji wa Barcelona tena au muda si mrefu hataendelea kuwa huko, na ni mchezaji ambaye tunamtaka,” alisema.
Kocha huyo alieleza kuwa Chicago Fire wanaamini usajili wa Lewandowski utakuwa mkubwa ndani na nje ya uwanja na jamii kubwa ya Wapolandi waliopo Chicago watafurahi kumuona nyota huyo akiitumikia timu hiyo.
“Tunaamini huu ungekuwa usajili mkubwa sana kwa klabu, kwa jiji la Chicago na kwa MLS (Ligi Kuu Marekani) nzima,” alisema.
Lewandowski pia anaripotiwa kuvutiwa na Manchester United pamoja na klabu kadhaa kutoka Saudi Arabia, huku uamuzi wa mwisho kuhusu hatma yake ukitarajiwa kufanyika baada ya Kombe la Dunia 2026.