Chelsea yamtoa machozi Thiago Silva, mashabiki wamuunga mkono
Muktasari:
- Silva (41), ambaye ni gwiji wa klabu hiyo, alikuwepo Stamford Bridge akitokea nchini Ureno. Hata hivyo, kile alichokishuhudia uwanjani kiliacha taswira ya huzuni na kukata tamaa usoni kwake.
LONDON, ENGLAND: MAPENZI ya Thiago Silva kwa klabu yake ya zamani, Chelsea, yameonekana kumpa maumivu makali baada ya kushuhudia vijana hao wa London wakisulubiwa nyumbani dhidi ya Nottingham Forest jana Jumatatu, Mei 04, 2026.
Silva (41), ambaye ni gwiji wa klabu hiyo, alikuwepo Stamford Bridge akitokea nchini Ureno. Hata hivyo, kile alichokishuhudia uwanjani kiliacha taswira ya huzuni na kukata tamaa usoni kwake.
Chelsea ilikubali kichapo cha fedheha cha mabao 3-1 dhidi ya Forest, likiwa ni pigo la sita mfululizo kwa upande wa mechi za Ligi ya EPL. Matokeo hayo yanaiacha ‘The Blues’ katika nafasi ya tisa, ikiwa pointi tatu tu mbele ya Newcastle iliyo katika nafasi ya 13, huku zikisalia mechi tatu pekee msimu huu.
Akiwa ameketi na mwanawe, Isago (anayechezea Akademi ya Chelsea), Silva alionekana kwenye kamera akiwa ameshika kichwa na kusugua macho kwa uchungu.
Baada ya kushinda taji la ligi nchini Ureno akiwa na FC Porto, tofauti ya kiwango cha kati cha klabu yake ya sasa na udhaifu uliokuwa uwanjani ulimfanya aonekane mwenye kuchukizwa zaidi.
Mashabiki wa Chelsea mtandaoni wameonyesha hisia zao kutokana na picha za Silva, huku mmoja akiandika kwenye mtandao wa X kwamba: "Fikiria unarudi klabuni kwako kisha unamuona Tosin uwanjani kama mbadala wako! Hata mimi ningelia."
Licha ya wamiliki Todd Boehly and Clearlake Capital kutumia zaidi ya pauni bilioni 1.5 kununua wachezaji wapya, hali ya Chelsea inaonekana kuzidi kuwa mbaya kuliko msimu wa 2023-24 wakati Silva akiondoka chini ya Mauricio Pochettino.
Takwimu zinaonyesha kuwa, kwa kiwango cha sasa, Chelsea inatajwa kuwa miongoni mwa timu zenye kiwango kibaya zaidi kwenye Ligi ya EPL.
Uwepo wa Silva na aliyekuwa kocha wa timu hiyo (na sasa kocha wa England), Thomas Tuchel, uliwakumbusha mashabiki wa Chelsea nyakati za dhahabu walizotwaa taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya mwaka 2021, nyakati ambazo kwa sasa zinaonekana kuwa ndoto.
Shabiki mmoja alisema: "Kile ambacho macho yake yameona, mdomo wake hauwezi kusema."