Chelsea imemfanyia hili Sterling
Muktasari:
- Chelsea ilisaini wachezaji wengi wapya dirisha lililopita la majira ya kiangazi, ikiwemo Joao Pedro, Jamie Gittens, Jorrel Hato, Liam Delap na Alejandro Garnacho.
LONDON, ENGLAND: BAADA ya kushindwa kupata timu dirisha lililopita la majira ya kiangazi, winga wa Chelsea na England Raheem Sterling anatarajiwa kukaa nje na kufanya mazoezi ya peke yake hadi Januari na ataangalia timu nyingine ya kujiunga nayo.
Chelsea ilisaini wachezaji wengi wapya dirisha lililopita la majira ya kiangazi, ikiwemo Joao Pedro, Jamie Gittens, Jorrel Hato, Liam Delap na Alejandro Garnacho.
Mbali ya kusajili, pia iliwaondoa wachezaji wengi ili kuweka sawa vitabu vyao vya mahesabu na kuwaingiza katika mfumo wale iliowasajili kwa ajili ya kuwatumia msimu huu.
Hata hivyo, Sterling hakupata klabu mpya, ingawa alihusishwa na Fulham na Crystal Palace saa za mwisho za dirisha la uhamisho.
Kutokana na hilo, Sterling anatarajiwa kufanya mazoezi mbali na kikosi cha kwanza cha Chelsea hadi dirisha la Januari.
Hayo ni kwa mujibu wa tovuti ya The Times, inayoeleza uhamisho wa kwenda nje ya England nchi kama Uturuki au Saudi Arabia hauwezi kufanyika kwa sasa kwani mchezaji mwenyewe anataka kubakia EPL.
Kutokana na hilo atalazimika kuwa nje ya kikosi kwa miezi kadhaa kabla ya Januari kwani Kocha Enzo Maresca hana mpango wa kumtumia.
Maresca hajumuishi mchezaji huyo, 30, katika mipango yake na hakuthibitisha kama wachezaji ambao wanafanya mazoezi kando na kikosi cha kwanza katika kambi ya mazoezi ya klabu watarudishwa ikiwa watashindwa kupata timu.
“Hakuna wazo la kuwarudidha kwa sasa, Sijui nini tutafanya juu yao. Unajua hawako nasi kwa sasa. Wanafanya mazoezi kwa wakati tofauti, katika uwanja tofauti. Kwa hivyo sina jibu lolote. Tutaona. Dirisha litakapofungwa, tutaamua.”
Sterling, ambaye alijiunga na Chelsea kutoka Manchester City kwa Pauni 47.5 milioni mwaka 2022, ni miongoni mwa wachezaji wanaopokea mshahara mkubwa zaidi Chelsea, akipokea Pauni 300,000 kwa wiki.