Chelsea hali si shwari, idadi ya majeruhi inaongezeka
Muktasari:
- Kiungo huyo wa kimataifa wa Argentina ameondoka kwenye kambi ya timu ya taifa na kurudi London kutokana na uvimbe kwenye goti lake la kulia.
LONDON, ENGLAND: CHANGAMOTO ya majeruhi Chelsea imezidi kuongezeka katika kipindi hiki cha mapumziko ya kimataifa baada ya kiungo wao Enzo Fernandez kulazimika kuondolewa katika kikosi cha timu ya taifa Argentina.
Kiungo huyo wa kimataifa wa Argentina ameondoka kwenye kambi ya timu ya taifa na kurudi London kutokana na uvimbe kwenye goti lake la kulia.
Fernandez amekuwa mchezaji muhimu sana Chelsea tangu msimu uliopita na msimu huu kwenye eneo la kiungo.
Mchezaji mwenzake katika eneo hilo, Moises Caicedo naye alipatwa na majeraha akiwa na kikosi cha Ecuador na alilazimika kupumzishwa.
Enzo huenda akakaa nje kwa muda usiopungua wiki moja na anaweza akarejea uwanjani kuitumikia Chelsea katika mechi ya Ligi Kuu England dhidi ya Nottingham Forest Jumamosi ya wiki hii.
Kwa sasa Chelsea inawakosa mastaa wake muhimu kama Joao Pedro, Reece James, Cole Palmer na Caicedo ambao wote wanaumwa lakini kuna uwezekano baadhi yao wakacheza mechi za wikiendi hii.
Romeo Lavia na Wesley Fofana, ambao wanadaiwa kuwa na hali nzuri baada ya kuwa nje kwa muda kutokana na majeraha, wanaweza kuungana na timu katika mechi dhidi ya Forest lakini hakuna uhakika wa asilimia mia.
Ikiwa Fernandez atashindwa kucheza mechi dhidi ya Forest, mbadala wake anaweza kuwa kiungo mwenzake wa Argentina, Facundo Buonanotte.
Trevoh Chalobah atarudi wikiendi hii baada ya adhabu yake kuisha, huku Tosin Adarabioyo, Andrey Santos na Palmer wakitarajiwa kuendelea kukosekana.
Chelsea pia itamkosa kocha wake Enzo Maresca ambaye anatumikia adhabu, hivyo atakayesimama katika benchi atakuwa ni Willy Caballero.
Hii ni baada ya kocha huyo wa kimataifa wa Italia kupewa kadi ya njano ya pili dhidi ya Liverpool kwa kukimbia kwenye mstari wa pembeni na kusherehekea bao la dakika za mwisho la Estevao.