Chelsea akili kubwa kwa Sancho
Muktasari:
- Sancho ambaye alijiunga na Man United mwaka 2021 kwa Pauni 73 milioni akitokea Borussia Dortmund amekuwa na wakati mgumu katika viunga hivyo hadi sasa.
LONDON, ENGLAND: CHELSEA inadaiwa kutumia akili kubwa katika makubaliano yao na Manchester United juu ya uhamisho wa mkopo wa Jadon Sancho ambapo wameweka kipengele kitakachowazuia kumnunua mazima mwinga huyo.
Sancho ambaye alijiunga na Man United mwaka 2021 kwa Pauni 73 milioni akitokea Borussia Dortmund amekuwa na wakati mgumu katika viunga hivyo hadi sasa.
Msimu uliopita aliingia katika mgogoro na kocha wake Erik ten Hag hali iliyosababisha kutolewa katika timu na kupelekwa kwa mkopo Dortmund kabla ya kurejeshwa baada ya msimu kumalizika.
Baada ya kurejeshwa iliwekwa wazi kwamba wawili hao wamemaliza tofauti zao lakini cha kushangaza kabla ya dirisha kufungwa, Sancho alitangazwa kujiunga na Chelsea kwa mkopo wa msimu mmoja.
Katika mkataba huo, imeelezwa kuna kipengele kinachoitaka Chelsea kumnunua kwa lazima ifikapo mwisho wa msimu ambapo watatakiwa kutoa kati ya Pauni 20 hadi 25 milioni.
Hata hivyo, Chelsea ilijaribu kujiweka salama kwa kuingiza kipengele ambacho kitawauzia kumsajili staa huyo mazima.
Kwa mujibu wa mwandishi wa gazeti la The Telegraph, James Ducker , Chelsea italazimika kumnunua Sancho kutoka Man United ikiwa tu itamaliza katika nafasi 14 za juu kwenye msimamo wa Ligi Kuu England, hivyo ikiwa tofauti Chelsea haitokuwa na ulazima wa kumsajili.
Mtaalamu wa masuala ya uhamisho Fabrizio Romano naye aliandika kwenye kurasa zake za mitandao ya kijamii: “Jadon Sancho, Chelsea na Man Utd walisaini nyaraka zote na makubaliano yamekamilika kwa asilimia mia, mkataba huo wa mkopo utawalazimu Chelsea kumnunua mazima ikiwa itamaliza katika nafasi 14 za juu kwenye msimamo wa EPL. Ada inaanzia Pauni 20 milioni hadi 25M.”