Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Che Malone aongoza USM Alger ikibeba Kombe la Shirikisho Afrika

Muktasari:

  • Dakika 90 za mchezo zimemalizika kwa wenyeji Zamalek kuibuka na ushindi wa bao 1-0, fainali ikipigwa Mei 16, 2026 kwenye Uwanja wa Kimataifa wa Cairo nchini Misri, mfungaji akiwa mshambuliaji Oday Dabbagh kwa penalti dakika ya tano.

BEKI wa zamani wa Simba, Che Malone Fondoh, amefanikiwa kufuta machozi, akibeba ubingwa wa Kombe la Shirikisho Afrika akiwa na kikosi cha USM Alger kutoka Algeria huku akiongoza kitakwimu kwa safu ya ulinzi ya timu hiyo.

Kilichombeba Che Malone ni kwamba, amecheza mechi zote 14 za Kombe la Shirikisho Afrika msimu huu kwa dakika 1,260 bila ya kufanyiwa mabadiliko huku akifunga bao moja hatua ya makundi dhidi ya FC San Pedro. Kwa wachezaji wa safu ya ulinzi ya timu hiyo, hakuna aliyefanya hivyo zaidi yake, huku Hocine Dehiri anayecheza naye beki wa kati, licha ya kufanikiwa kucheza mechi zote kama Che Malone, lakini hana bao wala asisti.

Katika fainali hiyo, dakika 90 zimemalizika kwa wenyeji Zamalek kuibuka na ushindi wa bao 1-0, fainali ikipigwa Mei 16, 2026 kwenye Uwanja wa Kimataifa wa Cairo nchini Misri, mfungaji akiwa mshambuliaji Oday Dabbagh kwa penalti dakika ya tano.

Hata hivyo, bao hilo halikutosha kuipa ubingwa Zamalek ambapo ikayafanya matokeo ya jumla kusomeka 1-1 kufuatia USM Alger kupata ushindi kama huo kwenye fainali ya kwanza nyumbani, wiki iliyopita.

Matokeo hayo yakaipeleka mechi hiyo kwenye mikwaju ya penalti na USM Alger kufanikiwa kushinda kwa penalti 8-7, Zamalek ikikosa moja kupitia kiungo na nahodha wake Mohammed Shehata kupaisha penalti yake.

Che Malone ambaye ni beki tegemeo wa USM Alger, amefanikiwa kufuta machozi baada ya kulikosa taji hilo akiwa Simba msimu uliopita lililochukuliwa na RS Berkane.

Mbali na mafanikio hayo ya CAF, pia msimu huu Che Malone ameshinda Kombe la Algeria, akicheza mechi tano za mashindano hayo kati ya sita, huku pia Ligi Kuu ya Algeria akicheza mechi 12 kati ya 23. Jumla msimu wake wa kwanza kikosini hapo, Che Malone amecheza mechi 32 kwa dakika 2,860.

Kwenye mechi mbili za fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika msimu huu, Che Malone raia wa Cameroon, ameonyesha kiwango bora akiwadhibiti vyema washambuliaji wa Zamalek, waliokuwa wanacheza mbele ya mashabiki wao.


PENALTI ZILIVYOTOA MSHINDI

Katika penalti, tano za kwanza zote zilijaa wavuni ambapo Zamalek iliyoanza kupiga, wafungaji wake walikuwa Abdallah El Said, Esho, Hossam Abdelmaguid, Nasser Mansy na Saiffedine Jaziri.

USM Alger nayo ikajibu mapigo kupitia Zakaria Draoui, Ahmed Khaldi, Saadi Radouani, Riad Benayad na Haithem Loucif.

Baada ya mzani kuwa sawa katika penalti tano za kwanza, zikaanza piga nikupige ndipo Zamalek wakafunga mbili zilifuatia kupitia Juan Alvina na Mohamed El Sayed, kisha Mohamed Shehata akakosa.

USM Alger ikafunga penalti tatu zilizofuatia wafungaji wakiwa Ilyes Chetti, Hocine Dehiri na Glody Likonza akaweka msumari ulioipa ubingwa timu hiyo.


MCHEZO ULIVYOKUWA

Zamalek ilitekeleza mpango wake vizuri tangu dakika za mwanzo. Dakika ya pili, Adam Kaied aliangushwa ndani ya eneo la hatari.

Oday Dabbagh alipiga penalti hiyo kwa utulivu na kumshinda kipa Oussama Benbot katika dakika ya tano. Bao hilo muhimu lilifuta mara moja kichapo cha 1-0 walichopata katika mchezo wa kwanza nchini Algeria na kubadilisha kabisa mwelekeo wa mchezo.

Zamalek walidhani wamepata bao la kuongoza kwa jumla ya mabao katika dakika ya 14. Mohamed Ismail aliunganisha mpira wavuni kwa kichwa lakini mwamuzi alilikataa bao hilo kwa madai ya kuotea.

Mambo yalikuwa magumu kwa Zamalek baada ya kipa wa kwanza, Mahdy Soliman kupata majeraha. Alitolewa dakika ya 30 na nafasi yake kuchukuliwa na Mohamed Awad.

Awad alionyesha ubora wake haraka kwa kuokoa mpira hatari uliopigwa kwa nguvu na Ahmed Khaldi muda mfupi kabla ya mapumziko.

Kipindi cha pili kilikuwa tofauti kabisa. Zamalek walirudi nyuma kulinda uongozi wao na kuwapa USM Alger nafasi ya kushambulia kwa nguvu.

USM Alger walitawala mchezo wakipiga mashuti tisa kufikia dakika ya 70 huku Zamalek wakifanya jaribio moja pekee. Khaldi, aliyefunga katika mchezo wa kwanza, aliendelea kuwa tishio kubwa na kukosa bao kwa tofauti ndogo mara mbili wakati wageni wakisaka bao muhimu la ugenini.

Kutafuta kurejesha udhibiti wa mchezo, dakika ya 60, benchi la Zamalek liliwaingiza Seifeddine Jaziri na Mohamed El Sayed.

Licha ya mabadiliko hayo, wenyeji walitegemea zaidi kujilinda ili kuhimili presha. Nasser Mansi alikaribia kuipa Zamalek ubingwa katika dakika ya 85 kwa kichwa kizuri lakini Benbot aliokoa kwa ustadi mkubwa na kuiweka salama USM Alger.

Baada ya dakika 90 kumalizika huku jumla ya mabao ikiwa 1-1, kanuni za CAF haziruhusu muda wa nyongeza katika hatua hiyo, hivyo timu hizo zikaenda moja kwa moja kwenye mikwaju ya penalti, ndipo USM Alger ikashinda 8-7 kufuatia Zamalek kukosa mkwaju wa nane uliopigwa na Mohamed Shehata.

Ubingwa huo ni wa pili kwa USM Alger katika Kombe la Shirikisho Afrika baada ya mwaka 2023 kuichapa Yanga kwa bao la ugenini kufuatia matokeo ya jumla kuwa 2-2. Mechi ya kwanza Dar es Salaam USM Alger ilishinda 2-1, nyumbani ikafungwa 1-0.

Kwa Zamalek, hilo lilikuwa pigo kwao kwani imepoteza fainali ya kwanza ya michuano hiyo baada ya kushinda 2018–19 na 2023–24.