Chamberlain afichua siri ya Arteta Arsenal
Muktasari:
- Oxlade-Chamberlain na Arteta walicheza pamoja Arsenal kwa miaka mitano, wakishinda Kombe la FA mara mbili. Ingawa ni zaidi ya miaka 10 iliyopita, kiungo huyo anadai aliona mapema kuwa Arteta alikuwa na uwezo wa kuwa kocha.
LONDON ENGLAND: MCHEZAJI wa zamani wa Arsenal, Alex Oxlade-Chamberlain amesema wachezaji wengi wa timu hiyo walikuwa wakimchukulia Mikel Arteta kuwa kocha kabla ya mechi kubwa licha ya Arsene Wenger kuwa ndiye kocha mkuu wakati huo.
Oxlade-Chamberlain na Arteta walicheza pamoja Arsenal kwa miaka mitano, wakishinda Kombe la FA mara mbili. Ingawa ni zaidi ya miaka 10 iliyopita, kiungo huyo anadai aliona mapema kuwa Arteta alikuwa na uwezo wa kuwa kocha.
Alifichua kuwa licha ya Wenger kuongoza timu, Arteta alikuwa akiongoza mikutano ya kuzungumzia mbinu kuhusu wapinzani kabla ya mechi kubwa.
Akizungumza kupitia kipindi cha In The Mixer, amesema: “Arteta alikuwa akiongoza mikutano hiyo kwa sababu unajua Wenger alikuwa akitokea kizazi tofauti. Tulipokutana na timu kubwa kama Manchester City au mechi muhimu, Mikel ndiye alikuwa bosi wetu. Mikel alikuwa na utaratibu wa kuwachambua wapinzani kwa kina.”
Oxlade-Chamberlain aliongeza kuwa kabla ya hapo, wachezaji walikuwa wanategemea maelezo ya jumla tu kutoka kwa Wenger, aliyekuwa akichora michoro kwenye ubao bila uchambuzi wa kina wa wapinzani.
Kwa sasa, Arteta ameendelea kuwa mmoja wa makocha bora katika Ligi Kuu England, akiwa karibu kuiongoza Arsenal kuchukua taji lao la kwanza la ligi hiyo baada ya muda mrefu. Hadi sasa, Arsenal inaongoza ligi kwa tofauti ya pointi tisa, huku pia ikiwa imefuzu robo fainali za Ligi ya Mabingwa na Kombe la FA.
Hivi karibuni, Oxlade-Chamberlain alirejea Arsenal kufanya mazoezi ili kujiweka fiti baada ya kuwa huru tangu aachane na Besiktas mwaka jana.