Jumba bovu… Kisa Kepa, Arteta hakwepi lawama
Muktasari:
- Kichapo cha Arsenal kimeibua mjadala mkubwa kutokana na maamuzi ya Arteta ya kuanza golini na Kepa badala ya Raya ambaye amekuwa muhimu zaidi langoni akiibeba Arsenal katika michuano mbalimbali inayoshiriki ikiwamo kuifikisha fainali katika kombe hili.
LONDON, ENGLAND: KITENDO cha kumwacha nje kipa David Raya na kumpanga Kepa Arrizabalaga katika fainali ya Kombe la Carabao kimechafua hali ya hewa kwa Kocha Mikel Arteta na kuonekana alifanya kosa kubwa sana.
Arsena ilicheza fainali ya Carabao dhidi ya Manchester City Jumapili na kuchapwa mabao 2-0 ya Nico O'Reilly ndani ya dakika nne na kupoteza ndoto zao za kubeba mataji makubwa ya England kama zilivyofanya Man chester United na Man City.
Kichapo cha Arsenal kimeibua mjadala mkubwa kutokana na maamuzi ya Arteta ya kuanza golini na Kepa badala ya Raya ambaye amekuwa muhimu zaidi langoni akiibeba Arsenal katika michuano mbalimbali inayoshiriki ikiwamo kuifikisha fainali katika kombe hili.
Kabla ya mechi, uamuzi huo ulionekana ni kama kamari na mashabiki waliokuwa na hofu waliona mapema tofauti ya viwango kati ya makipa hao, kabla ya dakika ya 60 kudhihirika baada ya Kepa kushindwa kudaka krosi ya Rayan Cherki na mpira kutua kwa Nico O'Reilly aliyefunga bao la kwanza kirahisi, kabla ya kupiga la pili dakika nne baadaye na kuipoteza Arsenal kabisa.
Mchambuzi Jamie Redknapp hakuwa na maneno ya kuficha, akisema: “Watu watasema ni uaminifu kwa sababu alicheza mechi za awali lakini ukweli Kepa si bora kuliko Raya, ndiyo maana ni kipa namba mbili.”
Redknapp alienda mbali zaidi kwa kumtupia lawama Arteta moja kwa moja akisisitiza: “Unapocheza fainali kubwa na unahitaji kushinda kwa nini uchague kipa wa pili? Hili ni kosa kubwa sana na lazima uwajibike.”
Kwa upande wake, Micah Richards alikubaliana na hoja hiyo akisema: “Tofauti ya kiwango kati ya Raya na Kepa ni kubwa na katika mechi kama hii lazima uchezeshe wachezaji wako bora.”
Ameongeza kwa kulinganisha na kipa wa City James Trafford: “Trafford aliletwa kama namba moja, yupo tayari kwa presha. Ndiyo maana aliokoa mashambulizi ya hatari mapema.”
Hata hivyo, wachambuzi hao walisisitiza tofauti kubwa ilikuwa kwenye maandalizi na City waliingia kushinda, wakati Arsenal walionekana kuwapa zaidi nafasi wachezaji badala ya ushindi.
Kipindi cha pili, timu ya Pep Guardiola iliongeza kasi na presha, ikitumia makosa ya Arsenal kama silaha ya kumaliza mchezo huo.
Mchambuzi Gary Neville hakusita kukosoa, akisema: “Hili ni kosa baya sana kwa kipa katika wakati mkubwa. City walifanya mashambulizi mfululizo na hatimaye wakapata wanachotaka.”
Neville aliongeza, “Nini kimewapata kipindi cha pili? Wamepotea kabisa. City walikuwa bora na walistahili ushindi.”
Katika mechi hiyo, Kepa alionekana kuchelewesha pasi na kukosa maamuzi ya haraka, jambo lililoongeza presha kwa safu ya ulinzi na kuifanya City kufanya mshambulizi mfululizo.
Baada ya mechi, Arteta alitetea uamuzi wake akisema: “Nilifanya uamuzi kwa kuangalia mchango wake katika mashindano haya na isingekuwa haki kumwacha nje.”
Kwa Arsenal, kipigo hiki kinaweza kuwa na athari kubwa zaidi kwani kinaibua maswali kuhusu ukomavu wa timu hiyo katika hatua za mwisho za mashindano makubwa huku wakiwa bado na nafasi ya kupigania taji la Ligi Kuu England, Kombe la FA na Ligi ya Mabingwa Ulaya.
4 – ARSENAL imepoteza fainali nne za mwisho za Carabao, na sasa ni rekodi mbaya zaidi ya kufika fainali bila kushinda kombe katika historia ya mashindano hayo.
15 – MANCHESTER City sasa ina ushindi 15 katika uwanja mpya wa Wembley kama timu ya ugenini tangu ulipofunguliwa 2007. Idadi kubwa zaidi kuliko timu yoyote ikivuka rekodi ya Chelsea ya ushindi mara 14.