Casemiro azibeba asisti za Bruno
Muktasari:
- Bruno ambaye ameendelea kutikisa Ligi Kuu ya England msimu huu wa 2025-2026 akionesha kiwango bora zaidi kiasi cha kufikia rekodi hiyo huku akipambana kuweka mpya kufuatia kuwa na mchezo mmoja wa mwisho, Casemiro ana mchango mkubwa.
MANCHESTER, ENGLAND: KATIKA ile rekodi ya nahodha wa Manchester United, Bruno Fernandes kufikisha asisti 20 msimu huu ndani ya Ligi Kuu England akiweka mzani sawa na Thierry Henry (msimu wa 2002-2003) na Kevin De Bruyne (2019-2020), nyuma yake kuna stori tamu inayomuhusu Casemiro.
Bruno ambaye ameendelea kutikisa Ligi Kuu ya England msimu huu wa 2025-2026 akionesha kiwango bora zaidi kiasi cha kufikia rekodi hiyo huku akipambana kuweka mpya kufuatia kuwa na mchezo mmoja wa mwisho, Casemiro ana mchango mkubwa.
Wakati Man United wikiendi iliyopita ikishinda 3-2 dhidi ya Nottingham Forest na Bruno kufikia rekodi hiyo, angeweza kuipiku na kuweka mpya kwani pasi zake nzuri za mwisho zilishindwa kutumiwa na Diogo Dalot na Bryan Mbeumo.
Casemiro ambaye ameaga klabuni hapo kwamba huu ndiyo msimu wake wa mwisho kuitumikia Man United, amekuwa anazitumia vizuri pasi za Bruno kwani ndiye mchezaji aliyefunga mabao mengi zaidi kupitia Mreno huyo.
Rekodi zinaonesha kwamba, Casemiro katika mabao yake tisa ndani ya Premier msimu huu, sita yametokana na asisti za Bruno.
Kiungo huyo mkongwe wa Brazil, amekuwa mnufaika mkuu, akifunga mabao dhidi ya Nottingham Forest, Bournemouth, Fulham, Newcastle, Aston Villa na Leeds.
Mwingine ni Benjamin Šeško ambaye katika mabao yake 11, kuna asisti nne za Bruno zilizotokea kwenye mechi dhidi ya Burnley, Fulham, Crystal Palace na Brentford.
Matheus Cunha pia amenufaika na asisti mbili alipofunga dhidi ya Aston Villa na Chelsea, sawa na Bryan Mbeumo aliyefunga bao la asisti ya 20 dhidi ya Nottingham Forest. Kabla ya hapo alifunga dhidi ya Manchester City.
Mason Mount naye anaingia kwa walionufaika na asisti mbili za Bruno, ilikuwa katika mechi dhidi ya Crystal Palace na Wolves.
Wengine waliopokea asisti moja kutoka kwa Bruno ni Harry Maguire (dhidi ya Liverpool), Matthijs de Ligt (Tottenham), Joshua Zirkzee (Crystal Palace) na Patrick Dorgu (Arsenal).
Bruno ambaye katika asisti 20 amezipata kwenye mechi 34 za Premier alizocheza msimu huu, takwimu zinaonesha zimechangia pointi 21 kwa Manchester United msimu huu, ambayo ni rekodi mpya kwa mchezaji mmoja katika msimu wa EPL.
Pia, ameweka rekodi ya klabu kwa kupiku asisti 15 za David Beckham za msimu wa 1999-2000.