Casemiro ‘amtolea uvivu’ Jamie Carragher
Muktasari:
- Casemiro amefunga mabao tisa katika mechi 33 za ligi akicheza nafasi ya kiungo mkabaji na ameshatangaza kwamba ataondoka mwisho wa msimu.
MANCHESTER, ENGLAND: NYOTA wa Manchester United, Casemiro, amemchana mchambuzi wa soka Jamie Carragher kwa kauli yake ya dharau aliyoitoa mwaka 2024 alipomwambia kuwa astaafu kwa sababu kiwango chake kimeshuka.
Hata hivyo, kiungo huyo mkongwe sasa amewanyamazisha wakosoaji wake baada ya kurejea kwenye kiwango bora akiwa sehemu muhimu ya mafanikio ya kikosi cha Manchester United chini ya kocha Michael Carrick kilichofanikiwa kufuzu Ligi ya Mabingwa.
Casemiro amefunga mabao tisa katika mechi 33 za ligi akicheza nafasi ya kiungo mkabaji na ameshatangaza kwamba ataondoka mwisho wa msimu.
Hata hivyo, nyota huyo mwenye umri wa miaka 34 aliwahi kupitia kipindi kigumu hali iliyosababisha lejendi wa Liverpool, Carragher, mwaka 2024, kusema kuwa muda wa Casemiro kucheza soka la kiwango cha juu ulikuwa umefika mwisho.
Miaka miwili baadaye, Casemiro ambaye ni mshindi wa mataji matano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya ameonekana kuwa katika kiwango bora sana na amemjibu Carragher alipokuwa akifanya mahojiano na mchezaji wa zamani wa Man United, Rio Ferdinand, akisema:"Basi... hayo ni maoni yake. Ninayaheshimu lakini siyapendi kwa sababu ni ya dharau. Ni dharau kwangu. Kwa sasa watu wanazungumza kuhusu mimi hapa England na hata ukienda Hispania iko hivyo pia. Kila mtu anamkumbuka Casemiro, kila mtu ananikumbuka kule."
Kabla ya kujiunga na Man United, Casemiro aliitumikia Madrid kwa miaka minane na nusu akitwaa mataji mengi makubwa, yakiwemo matatu ya La Liga na matano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Mapema msimu huu, nyota huyo wa Brazil alithibitisha kuwa ataondoka Man United katika dirisha la majira ya kiangazi, licha ya baadhi ya mashabiki kutaka aongeze mkataba.
Ingawa Casemiro amemjibu Carragher, mchambuzi huyo tayari alishakubali kosa lake Februari mwaka huu ambapo amesema:" Sasa ni haki kusema kwamba soka halijamuacha,” amesema Carragher kupitia Sky Sports. “Casemiro ana haki kabisa kama akitaka kunijibu na kunirudishia maneno. Hongera kwake, anaonekana mchezaji tofauti kabisa.”