Casèmiro amaliza minong’ono, kutua Inter Miami
Muktasari:
- Ili kufanikisha mpango huo, kiungo huyo raia wa Brazil amekubali kushusha madai yake ya mshahara kuendana na bajeti ya klabu pamoja na kanuni za Ligi Kuu ya Marekani (MLS).
KIUNGO wa kati wa Manchester United, Casemiro, amefikia makubaliano binafsi ya kujiunga na klabu ya Inter Miami inayoshirikishi Ligi Kuu ya Marekami (MLS).
Nyota huyo mwenye umri wa miaka 34, amevutiwa na fursa ya kuishi katika jiji la Miami yeye na familia yake, pamoja na nafasi ya kucheza sambamba na gwiji Lionel Messi.
Ili kufanikisha mpango huo, kiungo huyo raia wa Brazil amekubali kushusha madai yake ya mshahara kuendana na bajeti ya klabu pamoja na kanuni za Ligi Kuu ya Marekani (MLS).
Hata hivyo, uhamisho huo unakabiliwa na ‘kiwingu’ cha kanuni za ligi hiyo, kwani klabu ya LA Galaxy bado inashikilia haki za usajili wa mchezaji huyo ndani ya MLS. Ili kukamilisha dili hili, Inter Miami inalazimika kuingia kwenye mazungumzo na Galaxy kulipa ada ya fidia kwa ajili ya kuchukua haki hizo.
Hatua hii imezua manung'uniko makubwa miongoni mwa klabu pinzani za MLS, ambazo hazijafurahishwa na jinsi Miami inayomilikiwa na David Beckham inavyoendelea kutumia nguvu yake ya kifedha na ushawishi wa kibiashara kuvutia mastaa wakubwa.
Kikwazo kingine kwa Inter Miami ni ukosefu wa nafasi ya mchezaji wa kundi maalum, kwani nafasi hizo tatu kwa sasa zinashikiliwa na Lionel Messi, Rodrigo De Paul na German Berterame.
Kutokana na hali hiyo, Casemiro atalazimika kusaini mkataba wa kawaida utakaomuingizia kiasi cha dola milioni 1.8 kwa msimu wa kwanza, isipokuwa kama mmoja wa wachezaji hao watatu wa sasa ataondoka klabuni hapo.
Hii inafuatia tangazo la Casemiro la kutaka kuondoka Manchester United tangu Januari 2026, licha ya kumaliza msimu kwa kiwango cha juu chini ya kocha Michael Carrick.
Wakati huohuo, Manchester United inajiandaa na mabadiliko makubwa kwenye safu yake ya kiungo majira ya kiangazi, huku Manuel Ugarte naye akitajwa kuwa njiani kuondoka Old Trafford.
Klabu hiyo inalenga kusajili angalau viungo wawili wapya na tayari imefanya mazungumzo na Ederson wa Atalanta pamoja na Mateus Fernandes wa West Ham.
Hata hivyo, Man United inakabiliwa na kibarua kigumu kumsajili Elliot Anderson wa Nottingham Forest, kwani mahasimu wao Manchester City wanaongoza mbio za kuwania saini ya mchezaji huyo kwa dau la pauni milioni 90 (Sh314.6 bilioni).