Carrick atia neno kuhusu dili la Rashford
Muktasari:
- Rashford mwenye umri wa miaka 28, kwa sasa yupo kwa mkopo katika klabu ya Barcelona baada ya pia kucheza kwa mkopo Aston Villa msimu uliopita.
MANCHESTER, ENGLAND: KOCHA wa muda wa Manchester United, Michael Carrick amesema hakuna uamuzi wowote uliofanyika katika klabu hiyo kuhusu mshambuliaji Marcus Rashford.
Rashford mwenye umri wa miaka 28, kwa sasa yupo kwa mkopo katika klabu ya Barcelona baada ya pia kucheza kwa mkopo Aston Villa msimu uliopita.
Mchezaji huyo aliondoka Old Trafford baada ya kile kinachodaiwa kuwa ni kutofautiana na kocha wa zamani Ruben Amorim, hali iliyosababisha kutokuwa na nafasi katika kikosi cha kwanza.
Mkataba wa Rashford huko Barcelona unakipengele cha kusajiliwa moja kwa moja kwa ada ya pauni 26 milioni lakini miamba hiyo ya Hispania bado haijafanya uamuzi wa kukumia fursa hiyo.
Kwa mujibu wa taarifa, Barcelona inaonekana kusita kulipa kiasi hicho, jambo linalofanya kuwepo na sintofahamu kuhusu mchezaji huyo.
Akizungumzia hali hiyo, Carrick alisema: “Kwa sasa hakuna uamuzi wowote uliofanywa. Mambo yatatakiwa kuamuliwa wakati utakapofika lakini hadi sasa bado hakuna kilichoamuliwa.”
Rashford amecheza mechi 43 akiwa Barcelona, akifunga mabao 12 na kutoa pasi 13 za mabao.