Carragher aipa Man City ubingwa Premier
Muktasari:
- Ligi Kuu England inatarajiwa kuanza Ijumaa ijayo kwa mchezo mkali wa Manchester United ambayo itavaana na Fulham kwenye Uwanja wa Old Trafford, huku mechi nyingi zikitarajiwa kupigwa Jumamosi na Jumapili.
Manchester, England: Mchambuzi mahiri wa soka nchini England Jamie Carragher, amesema bado anaamini kuwa Manchester City ina nafasi kubwa ya kutwaa tena ubingwa wa Ligi Kuu England kama ilivyofanya msimu uliopita.
Ligi Kuu England inatarajiwa kuanza Ijumaa ijayo kwa mchezo mkali wa Manchester United ambayo itavaana na Fulham kwenye Uwanja wa Old Trafford, huku mechi nyingi zikitarajiwa kupigwa Jumamosi na Jumapili.
Manchester City inapewa nafasi kubwa ya kutwaa ubingwa huo kutokana na kiwango cha juu ambacho imekionyesha kwenye ligi hiyo kwa kipindi cha hivi karibuni na endapo itautwaa basi itakuwa mara yao ya tano mfululizo.
Mchambuzi huyo ambaye alichapisha taarifa hiyo kwenye mtandao wake wa Instagram pia anasema Arsenal inaweza kumaliza kwenye nafasi ya pili kama ilivyokuwa msimu uliopita, huku akiamini kuwa kuna vita kubwa kwa timu ambazo zinaweza kumaliza nafasi nne za juu kutokana na nyingi uwezo wao kufanana.
Kwa mujibu wa mchambuzi huyo ambaye alifanikiwa kuichezea Liverpool ambayo kwa sasa inafundishwa na kocha Arne Slot, anaamini kuwa inaweza kumaliza kwenye nafasi ya tatu, huku akiipa Tottenham nafasi ya nne na Man United ya tano.
Pamoja na Aston Villa kufanikiwa kumaliza kwenye nne bora msimu uliopita, lakini bosi huyo anasema kuwa timu hiyo chini ya kocha Unai Emery itamaliza nafasi ya sita msimu huu.
Mashabiki wengi wameonekana kutokubaliana na utabiri huyo huku wakisema kuwa ni mapema sana kufanya hivyo kabla hata ligi haijaanza. Shabiki mmoja aliandika: "Nani anaweza kukubaliana na hiki anachosema? Nafikiri ni mapema sana kufanya hivi'.
Mwingine aliandika kuwa timu yenye uwezo wa kutwaa ubingwa huo msimu huu ni Manchester United:'Manchester United itatwaa ubingwa wa ligi msimu huu na sina sababu ya kusema hivi."
Mwingine akiandika: 'Liverpool itapata shida sana mzunguko wa pili wa ligi, nafikiri tunatakiwa kuwa na mashaka sana na hili."
Mechi za Jumamosi zitakuwa kama ifuatavyo Ipswich dhidi ya Liverpool, Arsenal dhidi ya Wolves, Everton itavaana na Brighton, Newcastle dhidi ya Southampton, Nottigham Forest watawaalika Bournemouth, West Ham dhidi ya Aston Villa.
Huku Jumapili kukiwa na michezo miwili, Brentford dhidi ya Crystal Palace na Chelsea dhidi ya Man City.