CAF yazipiga rungu zito Senegal, Morocco kwa utovu wa nidhamu AFCON
Muktasari:
- Senegal ilitwaa ubingwa wa AFCON 2025 baada ya kuibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Morocco katika mechi ya fainali iliyochezwa jijini Rabat, Morocco, Januari 18, 2026.
Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) limetoa adhabu kali kwa vitendo vya utovu wa nidhamu vilivyoonyeshwa katika mechi ya Fainali ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) 2025 baina ya timu zao za taifa Januari 18, 2026.
Adhabu hizo ni faini kwa mashirikisho yote mawili zilizoenda sambamba na vifungo pamoja na faini nzito kwa Kocha Mkuu wa Senegal, Pape Thiaw na baadhi ya wachezaji wa timu zote mbili.
"Kumfungia Pape Bouna Thiaw, Kocha Mkuu wa Timu ya Taifa ya Senegal, kwa michezo mitano rasmi ya CAF kwa tabia zake zisizo za kiuanamichezo vilivyovunja kanuni zz nidhamu za CAF za mchezo wa kiungwana na maadili na kuuingiza mchezo kwenye utata.
"Pape Bouna Thiaw pia ametozwa faini ya Dola 100,000 (Sh256 milioni)," imefafanua taarifa ya CAF.
Taarifa hiyo imefafanua kuwa wachezaji wa Senegal, Iliman Ndiaye na Ismaila Sarr kila mmoja amefungiwa michezo miwili rasmi ya CAF kwa utovu wa nidhamu wa kumshambulia Refa wa mchezo.
Shirikisho la Mpira wa Miguu Senegal (FSF) lenyewe limepewa adhabu ya faini kiasi cha Dola 615,000 (Sh1.6 bilioni) kwa makosa matatu ambayo ni vurugu za mashabiki wa timu ya taifa ya nchi hiyo, vitendo vya utovu wa nidhamu vya wachezaji na maofisa wa benchi la ufundi la timu yao kwenye fainali hiyo pamoja na wachezaji wake watano kuonyeshwa kadi za njano.
Shirikisho la Mpira wa Miguu Morocco (FRMF) lenyewe limetozwa faini ya Dola 315,000 (Sh806 milioni) kwa makosa matatu.
Kosa la kwanza ni utovu wa nidhamu wa waokota mipira, utovu wa nidhamu wa wachezaji na maofisa wa benchi lake la ufundi kwa kuvamia eneo la VAR na kuzuia refa kufanya kazi yake pamoja na mashabiki wake kutumia tochi za mionzi ambazo haziruhusiwi.
Nahodha wa Morocco, Achraf Hakimi amefungiwa michezo miwili ambapo moja imesogezwa mbele kwa mwaka mmoja kutokana na vitendo vyake visivyo vya kiuanamichezo alivyoonyesha katika mechi hiyo.
Mshambuliaji Ismail Saibari wa Morocco, amefungiwa kucheza idadi ya mechi tatu rasmi za CAF na kutozwa faini ya Dola 100,000 (Sh256 milioni) kwa kosa la utovu wa nidhamu.
Katika hatua nyingine, CAF imetupilia mbali pingamizi la Morocco iliyotaka Senegal ipokonywe ubingwa na ukabidhiwe kwa timu yao la taifa ikidai Senegal ilifanya kosa la kugomea mchezo kinyume na kanuni ya 82 na 84 za AFCON.
CAF imeona pingamizi hilo halina mashiko na kuamua kuwa ubingwa wa Senegal ni halali.
Fainali hiyo iliyochezwa Jumapili, Januari 18, 2025 iliingia doa katika dakika za majeruhi za muda wa kawaida wa mchezaji baada ya kundi kubwa la wachezaji na maofisa wa benchi la ufundi la Senegal wakiongozwa na Kocha Thiaw kugoma kwa muda kabla ya baadaye kuamua kuendelea na mech.
Thiaw aliwaamuru wachezaji wake kutoka nje ya uwanja kufuatia uamuzi wa Refa Jean-Jacques Ndala kuamuru penalti kwenda langoni mwao baada ya Brahim Diaz kufanyiwa faulo na Malick Diouf.
Hata hivyo nyota wa Senegal, Sadio Mane alionekana kutokubaliana na uamuzi wa kuondoka uwanjani ambapo alionekana akiwashawishi wenzake kuendelea na mchezo.
Uamuzi wa Senegal kurejea uwanjani na kuendelea na mchezo, ulikuwa na faida kwa upande wao kwani Morocco walikosa mkwaju huo wa penalti uliopigwa na Brahim Diaz na baadaye ikatwaa ubingwa kwa ushindi wa bao 1-0 lililofungwa na Pape Gueye.