Bukayo Saka ni bosi mpya mjini

LONDON, ENGLAND. KAZI nzuri inalipa wanasema. Unataka kujua hilo, hebu mcheki Bukayo Saka.
Mavitu yake matamu kabisa ya msimu huu yamewafurahisha Arsenal na kuamua kumpa dili jipya linaloendana na mzigo anaopiga uwanjani.

Na sasa, winga huyo Mwingereza amesaini mkataba wa miaka minne wa kuendelea kuitumikia klabu ya Arsenal yenye maskani yake huko Emirates.
Kocha wa Arsenal, Mikel Arteta hakutaka kuchelewesha muda katika kuhakikisha anabaki na huduma ya mchezaji huyo kwa muda mrefu baada ya kusikia klabu nyingine kama Manchester City zikienza kupiga hesabu za kwenda kunasa saini yake.
Katika msimu huu, Saka mwenye umri wa miaka 22, alifunga mabao 14 na kuasisti mara 11.

Baada ya kusaini dili jipya, Saka alisema hivi: “Nina furaha sana. Kulikuwa na mazungumzo ya muda mrefu, lakini sasa nitaendelea kubaki hapa. Nadhani hii ni klabu sahihi, ni mahali sasa kwa ajili ya kupiga hatua ya juu zaidi. Ni klabu nzuri, ona tulipo kwa sasa.
“Kwangu mimi, muhimu ni kufanikiwa mambo binafsi. Ni jinsi gani najiongeza mwenyewe katika kufikia matarajio ya kila mchezo wiki moja hadi nyingine. Nipo na watu sahihi walionizunguka ikiwamo familia yangu, mazoezini, wachezaji wenzangu na benchi la ufundi.

“Nadhani nina kila kitu ninachohitaji kuwa mchezaji bora kwa kadri ninavyoweza na hilo ndilo lilolonifanya kuwa na furaha ya kubaki hapa kwa sababu naamini nitafanikiwa mambo makubwa zaidi.”
Ushajiuliza kwamba kwenye mkataba huo mpya wa Saka, analipwa kiasi gani na Arsenal?
Na kinachoelezwa ni kwamba Saka sasa atakuwa mchezaji anayelipwa mshahara mkubwa zaidi huko kwenye kikosi cha Arsenal kwa mujibu wa Daily Mail. Awali staa huyo alikuwa akilipwa Pauni 70,000 kwa wiki, kwa mujibu wa Capology.

Lakini, kwa dili lake jipya, analipwa karibu Pauni 300,000 kwa wiki, ikiwa ni zaidi ya mara nne ya kiwango alichokuwa akilipwa awali.
Kwa urefu wa mkataba wake huo wa miaka minne, Saka ataweka kibindoni mkwanja wa Pauni 75 milioni.
Kwa dili hilo jipya linamfanya Saka kuwamo kwenye orodha ya wanasoka wanaolipwa kibosi zaidi kwenye Ligi Kuu England.
Kwa sasa, supastaa wa Manchester City, Kevin De Bruyne ndiye mchezaji anayeshika namba moja kwa kulipwa mshahara mkubwa zaidi kwenye Ligi Kuu England, ambapo Mbelgiji huyo kwa huduma yake anayotoa huko Etihad, kwa mwaka analipwa Pauni 20.8 milioni.

Kipa wa Manchester United, David de Gea hayupo mbali sana kwenye nafasi ya pili, lakini Mhispaniola huyo mkataba wake utafika tamati mwisho wa msimu huu na kama atahitaji kuendelea kubaki Old Trafford basi atalazimika kushusha mkataba wake kwa kiwango kikubwa. De Gea analipwa Pauni 19.5 milioni.
Kwenye nafasi ya tatu, Erling Haaland analipwa Pauni 19.5 milioni kwa mwaka, wakati Jadon Sancho anapokea Pauni 18.2 milioni, Mohamed Salah Pauni 18.2 milioni, Raphael Varane – Pauni 17.6 milioni, Raheem Sterling – Pauni 16.9 milioni, Casemiro – Pauni 15.6 milioni, Jack Grealish – Pauni 15.6 milioni, Kalidou Koulibaly – Pauni 15.3 milioni, N’Golo Kante – Pauni 15 milioni, Bukayo Saka – Pauni 15 milioni, Gabriel Jesus – Pauni 13.7 milioni, Anthony Martial – Pauni 13 milioni na John Stones – Pauni 13  milioni.

Kiungo mkata umeme wa Chelsea, N’Golo Kante mshahara wake wa sasa atakuwa analipwa sawa na kiwango kama atakacholipwa Saka kwa sasa, lakini naye mkataba wake huko Stamford Bridge utafika tamati mwishoni mwa msimu huu.

Hii hapa orodha ya mastaa 20 wanaolipwa kibosi zaidi kwenye Ligi Kuu England
20. Virgil van Dijk - Liverpool, Pauni 220,000 kwa wiki
19. Rodri - Man City, Pauni 220,000 kwa wiki
18. Phil Foden - Man City, Pauni 225,000 kwa wiki
17. Bruno Fernandes - Man United, Pauni 240,000 kwa wiki
16. Anthony Martial - Man United, Pauni 250,000 kwa wiki
15. John Stones - Man City, Pauni 250,000 kwa wiki
14. Reece James - Chelsea, Pauni 250,000 kwa wiki
13. Gabriel Jesus - Arsenal, Pauni 265,000 kwa wiki
12. N'Golo Kante - Chelsea, Pauni 290,000 kwa wiki
11. Bukayo Saka - Arsenal, Pauni 290,000 kwa wiki
10. Kalidou Koulibaly - Chelsea, Pauni 295,000 kwa wiki
9. Casemiro - Man United, Pauni 300,000 kwa wiki
8. Jack Grealish - Man City, Pauni 300,000 kwa wiki
7. Raheem Sterling - Chelsea, Pauni 325,000 kwa wiki
6. Raphael Varane - Man United, Pauni 340,000 kwa wiki
5. Jadon Sancho - Man United, Pauni 350,000 kwa wiki
4. Mohamed Salah - Liverpool, Pauni 350,000 kwa wiki
3. David de Gea - Man United, Pauni 375,000 kwa wiki
2. Erling Haaland - Man City, Pauni 375,000 kwa wiki
1. Kevin De Bruyne - Man City, Pauni 400,000 kwa wiki