Brighton haitishwi Carlos Baleba kuondoka
Muktasari:
- Kiungo Carlos Baleba ni jina la staa mwingine anayeshusishwa na mpango wa kuondoka Amex kwenye dirisha hili la uhamisho wa majira ya kiangazi.
LONDON, ENGLAND: BOSI wa Brighton, Fabian Hurzeler hana hofu ya kuwapoteza mastaa wao kwa sababu ana uhakika wa kutafuta suluhu ya timu kuendelea kufanya vizuri baada ya kuuza wachezaji wao nyota.
Kiungo Carlos Baleba ni jina la staa mwingine anayeshusishwa na mpango wa kuondoka Amex kwenye dirisha hili la uhamisho wa majira ya kiangazi.
Manchester United ndiyo inayohusishwa na Baleba, ikitaka saini yake baada ya kumsajili straika Benjamin Sesko kwa Pauni 74 milioni, anayekwenda kuungana na washambuliaji wengine, Bryan Mbeumo na Matheus Cunha.
Brighton imeshamuuza Joao Pedro kwenye dirisha hili la majira ya kiangazi na iliachana na viungo wengine matata kama Alexis Mac Allister na Moises Caicedo kwa miaka ya hivi karibuni.
Wakati kocha huyo wa Brighton akidai kwamba hawezi kuiondoa timu hiyo kwenye kundi la timu zinazouza wachezaji wake, hiyo inaipa Man United matumaini.
“Sisi kama klabu siku zote tumekuwa tukitafuta suluhisho na nina uhakika huko baadaye tutapata suluhu pia ya matatizo mengine,” alisema Hurzeler.
“Tumeonyesha sisi si klabu ya kuuza wachezaji kwa bei ndogo. Tumekuwa na ofa nyingine pia, kubwa tu kwa ajili ya Kaoru Mitoma na wachezaji wengine. Tunaonyesha si klabu inayouza wachezaji kirahisi.”
Hurzeler anaamini klabu hiyo itaweza kukabiliana na changamoto zote zitakazowakabili kutokana na kuuza wachezaji wao bora.