Brazil, Misri, Argentina zakaa pazuri

Mchezaji wa England, Saido Berahino akipiga shuti huku mchezaji wa Argentina, Alan Ruiz (kushoto) akijaribu kuzuia wakati wa mechi ya kombe la Dunia kwa U-20 Mechi iliyochezwa kwenye uwanja wa Atanasio Girardot mjini Medellin, Colombia, juzi. Picha na AFP
MEDELLIN, Colombia TIMU ya Brazil ilichapa Austria 3-0, huku Argentina wakilazimishwa suluhu na watani zao England kwenye fainali za Kombe la Dunia kwa Vijana chini ya miaka 20 yanayoendelea nchini Colombia. Timu hizo mbili za Amerika Kusini na Hispania ndizo zinazopewa nafasi kubwa ya kutwaa taji hilo wakati michuano hiyo ikiwa kwenye hatua ya makundi. Katika mechi nyingine zilizochezwa Jumatatu, Misri ilijirekebisha na kupata ushindi wa bao 1-0 dhidi Panama kwenye Kundi E nao Mexico wameendelea ubabe kwa kuichapa Korea Kaskazini 3-0 kutoka Kundi F. Kiungo mchezaji wa Brazil, Philippe Coutinho alifunga bao moja na kututegeneza mengine mawili katika mchezo huo wa Kundi E. Henrique alifunga bao la kwanza kwa Brazil dakika ya 37, akimalizia krosi ya Oscar kabla ya Coutinho aliyeshiriki katika kutegeneza bao hilo naye kufunga la kwake kwa mkwaju wa penalti dakika 52 baada ya Danilo kuangushwa kwenye eneo la hatari. Kiungo huyo wa Inter Milan alitegeneza bao la tatu kwa kupitisha pasi nzuri kwa Casemiro, ambaye alimpigia pasi Willian aliyefunga kirahisi goli dakika 63. Brazil na Misri zinapointi nne baada ya mechi mbili za Kundi E, lakini timu hiyo ya Amerika Kusini wanaongoza kwa tofauti ya mabao. Timu mbili za juu katika kila kundi zinafuzu kwa hatua ya mtoano na zitaungana na timu nne ambazo zitakuwa washindi wa tatu bora. England imejifariji baada ya kupata suluhu na Argentina. Lakini sare hiyo imeifanya Argentina kufika pointi nne baada ya mechi mbili za Kundi F, zinazoweza kuwavusha hatua ya pili. England inahitaji ushindi kwenye mchezo wa mwisho dhidi ya Mexico ili kufuzu. Misri imejiweka kwenye nafasi nzuri ya kufuzu baada ya kuifunga Panama shukrani kwa Ahmed Hegazi aliyefunga bao pekee dakika ya 67. Mexico nayo ilipata ushindi mnono dhidi ya Korea Kusini. Sare yoyote dhidi ya England kwenye mchezo wa mwishi itatosha kuwavusha kwenye 16 bora. “Tunafirikilia kufanya kitu kikubwa zaidi hapa,” alisema kocha wa Mexico, Juan Carlos Chavez. “Tuna ndoto kubwa. Tunataka kucheza fainali.” Mexico ndiyo timu iliyofunga mabao mengi. Timu yao ya wakubwa ilitwaa Gold Cup, kwa kuifunga Marekani 4-2, pia timu ya Mexico ilitwaa Kombe la Dunia kwa vijana U17, kwa kuifunga Uruguay 2-0 katika fainali.