BRAZIL 2014: Majanga Ghana,Balotelli agombana na wenzake vyumbani

Muktasari:
- Boateng anadaiwa kumtukana kocha, Kwesi Appiah na Muntari amemtolea lugha chafu Mjumbe wa Black Stars, Moses Armah.
Brasilia, Brazil
NI majanga juu ya majanga. Baada ya kuwatimua wachezaji wake wawili kwa utovu wa nidhamu, Ghana ‘Black Stars’ jana Alhamisi ilifungwa na Ureno mabao 2-1 na kuaga rasmi fainali za Kombe la Dunia.
Ghana imewatimua, Sulley Muntari na Kevin Prince Boateng kwa utovu wa nidhamu.
Boateng anadaiwa kumtukana kocha, Kwesi Appiah na Muntari amemtolea lugha chafu Mjumbe wa Black Stars, Moses Armah.
Hata hivyo, kabla mchezo na Ureno, Muntari alikuwa na kadi mbili za njano ambazo zilimzuia kucheza mechi hiyo.
Beki wa Ghana, John Boye alijifunga dakika ya 31 alipotaka kuokoa mpira uliopigwa na Miguel Veluso wa Ureno.
Asamoah Gyan alivunja rekodi ya Roger Milla kwa kufunga bao la tano kwenye Kombe la Dunia alipounganisha kwa kichwa krosi ya Kwadwo Asamoah dakika 57.
Cristiano Ronaldo aliisumbua ngome ya Ghana na kupachika bao lake pekee katika fainali hizo dakika ya 80 baada ya kipa wa Ghana, Dauda kuutema mpira.
Ghana na Ureno ziko Kundi G na zote zimetolewa wakati Ujerumani na Marekani zimefuzu katika kundi hilo. Ujerumani jana iliilaza Marekani bao 1-0, mfungaji akiwa ni Thomas Muller aliyefunga bao lake la nne katika fainali hizo.
Wakati Ghana ikikumbwa na hayo, hali si shwari katika Timu ya Taifa ya Italia.
Unajua kilichotokea baada ya Italia kufungwa bao 1-0 na Uruguay na kuziaga fainali za Kombe la Dunia?
Wakati wa mapumziko, straika Mario Balotelli aliyekuwa akibeba matumaini ya Wataliano na ambaye asili yake ni Ghana aligombana na wachezaji wenzake walipokuwa kwenye vyumba vya kubadilishia nguo wakijadiliana namna ya kuwakabili Uruguay.
Kutokana na ugomvi aliosababisha Balotelli, kocha Prandelli, aliamuadhibu kwa kumtoa kipindi cha pili kutokana na kuchukizwa na maneno makali aliyowatamkia wenzake wakati wa mapumziko.
Inadaiwa beki wa Italia na Klabu ya Juventus, Leonardo Bonucci, alimtaka Balotelli kutoka vyumbani baada ya wawili hao kutupiana lugha za matusi.
Sakata hilo liliingiliwa na kiungo, Daniele de Rossi, aliyetaka kumaliza tatizo kwa kujaribu kumtetea Balotelli kitu kilichoibua utata mkubwa kwani Bonucci hakupenda hilo.
Baada ya mechi hiyo, De Rossi aliwaponda mastaa waliogombana na kudai timu hiyo inahitaji wapambanaji wa uwanjani na si vinginevyo.