Bosi Brighton afichua ishu ya Baleba United
Muktasari:
- Man United ilihusishwa na kiungo huyo Mcamerooni kwenye dirisha lililopita la uhamisho wa majira ya kiangazi ambapo kocha Ruben Amorim alijaribu kuboresha kiungo yake.
LONDON, ENGLAND: BOSI wa Brighton, Tony Bloom amefichua kwamba aliwaambia Manchester United hakuna namna yoyote watamuuza kiungo wao Carlos Baleba.
Man United ilihusishwa na kiungo huyo Mcamerooni kwenye dirisha lililopita la uhamisho wa majira ya kiangazi ambapo kocha Ruben Amorim alijaribu kuboresha kiungo yake.
Brighton iliripotiwa kutaka Euro 120 milioni ili kumuuza Baleba, kiasi cha pesa ambacho Man United haikuwa tayari kulipa.
Mwenyekiti wa Brighton, Bloom alibainisha kitu kilichowafanya Man United kufuta mpango wa kumsajili kiungo huyo kwa sababu waliambiwa hauzwi.
Bloom alisema: “Sidhani kama Baleba jambo lake lilikuwa sakata. Kulikuwa na ofa kutoka Manchester United, na tuliwaambia mchezaji huyo hapatikani mwaka huu, wakaondoka.”
Baleba, 21, alibaki kwenye kikosi cha Brighton ambapo ana mkataba hadi 2028. Kama angeondoka basi angefuata nyayo za wakali Moises Caicedo, Marc Cucurella, Alexis Mac Allister, Leandro Trossard na Robert Sanchez, ambao wameachana na Brighton katika miaka ya karibuni.
Bloom alisema kwamba anaamini Brighton haiwezi kuhesabika kama klabu inayouza wachezaji wake. Miamba hiyo ya Ligi Kuu England imekuwa na mwanzo kupanda na kushuka kwenye kiwango chake msimu huu chini ya kocha Fabian Hurzeler.
Timu hiyo inashika nafasi ya 12 kwenye msimamo baada ya kushinda mechi mbili kati ya saba.