Ben White atibua hesabu za Arteta
Muktasari:
- Beki huyo wa kulia alikumbana na tatizo hilo la majeraha ya misuli kwenye kipindi cha kwanza katika mchezo wa ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Wolves kwenye Ligi Kuu England, Jumamosi iliyopita.
LONDON, ENGLAND: Beki wa Arsenal, Ben White atakuwa nje ya uwanja kwa muda usiopungua mwezi mmoja baada ya kupata maumivu ya misuli.
Beki huyo wa kulia alikumbana na tatizo hilo la majeraha ya misuli kwenye kipindi cha kwanza katika mchezo wa ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Wolves kwenye Ligi Kuu England, Jumamosi iliyopita.
White, 28, alifanyiwa vipimo vya kutambua ukubwa wa tatizo lake Jumapili iliyopita na anaweza kuwa nje ya uwanja kwa wiki nne au tano. Na hilo ni pigo kubwa kwa Kocha Mikel Arteta, ambaye kikosi chake kinakabiliwa na wachezaji wengi majeruhi, hasa kwenye safu ya ulinzi.
Beki Cristhian Mosquera atakuwa nje ya uwanja hadi mwezi ujao kutokana na kusumbuliwa na maumivu ya enka. Na Gabriel Magalhaes bado hajarudi mazoezini kutokana na kusumbuliwa na maumivu ya paja.
Kiraka Jurrien Timber anajiandaa kucheza kwenye beki ya kulia dhidi ya Everton, Jumamosi kutokana na kocha Arteta kuwa na uhaba wa mabeki licha ya beki wa kushoto, Riccardo Calafiori kuruhusiwa kucheza baada ya kumaliza adhabu yake.
White, ambaye alipata majeraha tofauti kabisa na yale ya mwanzo ambayo yalimfanya kuwa nje ya uwanja kwa muda mrefu kutokana na kuumwa goti. Wachezaji wengine wa Arsenal ambao ni majeruhi ni Kai Havertz na Max Dowman.
White alianzishwa kwenye kikosi cha Arsenal katika mechi tatu zilizopita za Ligi Kuu England na alicheza pia kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Club Brugge wiki iliyopita. Kwa jumla wake, msimu huu amecheza mechi 11 tu.